Helb: Waziri Amina akaangwa na maseneta
Na CHARLES WASONGA
MASENETA Alhamisi walimkaripia Waziri wa Elimu Amina Mohamed kwa kupendekeza kuwa polisi watatumika kuandama Wakenya ambao walifaidi kutokana na mikopo kutoka kwa Bodi ya Elimu ya Juu (Helb) lakini wamedinda kulipa.
Wametaja wazo hilo kama lisilofaa na kupendekeza kwamba serikali ibuni sera itakayotoa utaratibu wa kufutiliwa mbali kwa mikopo hiyo, kama ilivyofanyika kwa wakulima wa kahawa na chai.
Suala hilo liliibuliwa na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula ambaye alitaka Wizara ya Elimu kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.
Alipendekeza kuwa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu imwalike Waziri Mohamed ili aseme ni kwa nini atataka wale ambao hawajalipa wakamatwe na polisi ilhali wengi wao hawana ajira.
“Waziri wa Elimu anafaa kuitwa afike mbele ya kamati ya elimu ya bunge ili atoa mwanga kuhusu amri hii ambayo haizingatii masilahi wa wahitimu wengi ambao hawajapata ajira. Mbona mtu ambaye ambaye ameshindwa kulipa mkopo akamatwe na polisi kama mwizi ilhali hajapata uwezo wa kulipa deni la Helb?” Bw Wetang’ula akauliza.
Kutolipa
Bodi hiyo imedai kuwa kufikia sasa jumla ya watu 74,000 waliofaidi kutokana na mikopo yake hawajalipa jumla ya Sh7.2 bilioni, hatua ambayo inahujumu uwezo wake wa kutoa mikopo kwa wanafunzi wengine. Ufichuzi huu ulijiri Jumanne wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati wa Bodi hiyo wa Kati ya 2019 hadi 2023.
Seneta wa Nyeri Ephraim Maina alipuuzilia mbali amri hiyo huku akimkumbusha Waziri Amina kwamba mkopo huwa ni makubaliano kati ya watu wawili.
“Kutolipwa kwa mkopo sio kosa la uhalifu ambalo polisi watafaa kutumika kulishughulikia,” akasema.
Naye Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alisema pendekezo la Waziri Mohamed ni sawa nma kuadhibu masikini huku akiitaka Helb kusaka usaidizi wa mahakama ili kukomboa pesa hizo.
Naye Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alisema: “Badala ya kuwaadhibu vijana walipewa mkopo na kukosa kulipa kwa kukosa kazini, serikali inapasa kuwaandama wale waliopora pesa za Shirika la Vijana kwa Huduma kwa Taifa (NYS) na wezi wengine wa pesa za umma.”
Kwa upande wake Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja alifananisha amri hiyo na kutangazwa kwa vita dhidi ya vijana.
“Taifa ambalo linapigana na vijana wake ni taifa ambalo linajimaliza yenyewe. Kama bunge tunapasa kuwatetea vijana waliosoma lakini hawana ajira kwani wao ndio wadhamini wa mustakabali wa taifa hili,” akasema.
Seneta wa Nandi Samson Cherargei alimtaka Waziri Amina kusaka njia za kuwawezesha vijana kupata ajira ili waweze kulipa mikopo yao “badala ya kuwatisha”.
“Kama taifa tunapaswa kupanga matumizi ya rasilimali yetu kwa namna ambayo itachangia kuzalishwa kwa nafasi za kazi, sio kupanga namna ya kuwakamata vijna,” akasema.