Habari

HISTORIA: Kenya kutuma setlaiti ya kwanza kwenye sayari

May 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

KENYA inatazamia kuweka historia Ijumaa hii wakati setilaiti ya kwanza kuwahi kutengenezwa nchini itakapotumwa katika sayari.

Chombo hicho cha kuzunguka sayari kilitengenezwa na wanafunzi na watafiti wa Chuo Kikuu cha Nairobi kwa ushirikiano na shirika la teknolojia za sayari la Japan Space Agency (JAXA).

Naibu Chansela wa UoN, Prof Peter Mbithi (pichani), alisema mafanikio hayo ni dhihirisho la hatua kubwa zilizopigwa nchini kuhusu utafiti wa kiteknolojia ambao unaweza kuchangia katika maendeleo yatakayokuza uchumi wa kitaifa.

Setilaiti hiyo yenye ukubwa wa sentimita kumi kimchemraba itarushwa sayarini kutoka kwa kituo kilicho Japan, lakini Wakenya kadhaa watapewa nafasi kushuhudia matukio hayo katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo yatapeperushwa moja kwa moja.

“Kutakuwa na tukio Japan, katika sayari na hapa UoN. Kile kitakachofanyika Japan kitashuhudiwa na baadhi ya Wakenya ambao watakuwa huko.

Hapa tutakuwa na hafla katika ukumbi ambapo matukio yatapeperushwa moja kwa moja. Tunasubiri siku hiyo kwa hamu,” akaambia wanahabari Jumatatu.

Wale ambao wangependa kuhudhuria hafla hiyo katika ukumbi wa Chandaria ulio UoN bewa la jijini Nairobi watahitajika kutuma maombi kwenye tovuti ya chuo hicho na watafahamishwa kama wamebahatika kupata nafasi.

Prof Mbithi aliongeza kuwa setilaiti hiyo itatumiwa kukusanya deta kuhusu masuala mbalimbali muhimu kama vile mabadiliko ya hali ya anga, uhifadhi wa wanyamapori, utabiri wa hali ya hewa miongoni mwa mengine.

Alitoa wito kwa wadau wengine waungane nao ili kuimarisha zaidi utafiti kuhusu masuala ya sayari pamoja na kutia nguvu chombo hicho ili kifanikiwe kutimiza malengo yake.

Mkuu wa taasisi ya mafunzo ya uhandisi katika chuo hicho, Prof Jackson Mbuthia, alisema setilaiti hiyo yenye uzani wa kilo 14 itasafirishwa hadi kwenye sayari mwendo wa saa saba mchana Ijumaa.

“Huu ni mwanzo wa safari ambayo itawezesha Kenya kushiriki kwenye sayansi ya sayari. Ni mara yetu ya kwanza kupiga hatua hii lakini tunaamini ni muhimu katika ustawishaji wa sayansi nchini,” akasema.

Kulingana naye, sayansi ya sayari imechangia pakubwa kwa maendeleo ya mataifa makuu kiuchumi na hivyo basi Kenya itapata nafasi bora ya kunufaika kwa jinsi hiyo hiyo.

Mbali na JAXA, mradi huo pia ulishirikisha mchango kutoka kwa shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya Sayari (UNOOSA).