Historia MKenya akitunukiwa cheo ya Luteni Kanali katika Jeshi la Amerika
MZAWA wa Kenya anayehudumu katika Jeshi la Amerika Silvia Jemutai amepandishwa cheo na kuwa Luteno Kanali.
Jemutai, aliyezaliwa katika kijiji cha Kopsiya, Wadi ya Poror, eneo bunge la Eldama Ravine, Kaunti ya Baringo, alipokezwa cheo hicho kipya mnamo Novemba 14, 2025, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Fort Lee, jimbo la Virginia.
Familia na marafiki wa Mwanajeshi huyo kutoka Kenya na Amerika walihudhuria hafla hiyo ya kipekee.
Luteni Kanali Jemutai alisema amekiamua kutumia cheo hicho kumuenzi marehemu mamake, Jacqueline Alice Kirui, ambaye mwongozo wake ulimsaidia kufikia ufanisi huo.
Kupandishwa ngazi kwake kunamfanya kuwa mwanajeshi Mkenya wa cheo cha juu zaidi katika Jeshi la Amerika wakati huu.
“Huyu ni Meja Silvia Jemutai kutoka Kopsiya, Poror, Eldama Ravine. Alipandishwa cheo rasmi kuwa Luteni Kanali katika Jeshi la Amerika wakati wa sherehe iliyofanyika Novemba 14, katika Fort Lee, Virginia,” ikasema ujumbe uliochapishwa na Gotabgaa International kwenye mtandao wa Facebook mnamo Jumanne, Novemba 18, 2025.
“Pongezi Luteni Kanali Silvia Jemutai……… sasa Mkenya mwenye cheo cha juu zaidi katika Jeshi la Amerika, binti halisi wa Kenya…. fahari ya Kenya,” ujumbe huo ukaongeza.
Lakini jeshi la Amerika, afisa wa cheo cha Luteni Kanali husimamia kati ya wanajeshi 300 hadi 1,000 au anaweza kutwikwa wajibu mkubwa katika Makao Makuu ya Jeshi la Amerika.