HIVI PUNDE: Wanne kati ya saba walioteuliwa IEBC wapingwa kortini
HAMU ya Wakenya ya kuona Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeundwa huenda ikacheleweshwa kwa muda usiojulikana kufuatia maswali yanayoibuliwa kuhusu watu wanne kati ya saba walioteuliwa hivi majuzi na Rais William Ruto.
Kesi iliyowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi, inadai kuwa mwenyekiti aliyependekezwa, Bw Erastus Edung Ethekon, pamoja na makamishna wateule Hassan Noor Hassan, Mary Karen Sorobit na Anne Nderitu hawakuwa na sifa zinazohitajika kuomba kazi hiyo wala kuchaguliwa kuwa wanachama wa IEBC.
Sababu zilizotolewa ni upendeleo wa kisiasa unaoonekana wazi, kukiuka kanuni za kutoegemea upande wowote wa kisiasa, kushiriki siasa mwaka wa 2022, kuwa wanachama wa vyama vya kisiasa na kushindwa kuacha nyadhifa za serikali kabla ya uteuzi wao.
Waliteuliwa pamoja na Moses Mukwana, Francis Odhiambo na Fahima Abdalla kuwa makamishna. Kesi hii mpya imeibua kikwazo kingine wakati Bunge la Kitaifa inajiandaa kuwahoji watu hao saba walioteuliwa.
Ingawa kesi inawahusu wote saba, walalamishi wameelekeza lawama zaidi kwa hao wanne kuhusu ufaafu na uadilifu wao, na wanataka hatua ya Rais kufutwa.
Iwapo Bunge litaidhinisha uteuzi huo na mahakama ikubaliane na hoja dhidi ya wanne hao, IEBC haitaweza kuendesha shughuli zake.
Kulingana na stakabadhi za mahakama, majina mengine yaliyowasilishwa kwa Rais na Jopo la Uteuzi yalijumuisha Edward Katama Ngeywa, mwenye umri wa miaka 49 kutoka Kaunti ya Trans Nzoia anayeishi na ulemavu, aliyependekezwa kuwa mwenyekiti pamoja na Bw Ethekon.
Kwa nafasi za makamishna, jopo pia lilipendekeza Bw Phillip Kakai na Joseph Kyavoa.
Rais hakueleza ni kwa nini alikataa mapendekezo ya watatu hao, jambo ambalo pia limejumuishwa katika msingi wa kesi inayoendelea.
Kesi iliwasilishwa na Wakenya wawili, Bw Kelvin Roy Omondi na Boniface Mwangi, wanaotaka mahakama kuzuia watu hao saba kushikilia nyadhifa hizo.
Mawakili wao wanadai kuwa mashauriano na upinzani yalikuwa hitaji kulingana na Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa (NADCO) na Sheria ya IEBC (Marekebisho), 2024. Pia wamedai kuwa baadhi ya maeneo kama Ukambani hayakuwakilishwa.
“Uteuzi huu unakiuka Katiba kwa kuwa hauwakilishi jamii tofauti za Kenya, unawatenga watu wa makabila mengine na wenye ulemavu. Walioteuliwa walichaguliwa bila mashauriano yoyote ya awali na upinzani kama inavyohitajika,” wanasema.