Hofu ya Corona yatikisa Kenya
BENSON MATHEKA na CHARLES WASONGA
TAHARUKI imetanda nchini, Wakenya wakiwa na wasiwasi wa kuambukizwa homa hatari ya Corona kutokana na idadi kubwa ya raia wa China wanaoruhusiwa kuingia nchini.
Kufuatia hofu hiyo, serikali ilichukua hatua ya kupunguza wageni wanaoingia nchini moja kwa moja kutoka China hapo Ijumaa.
Hatua hii ilichukuliwa baada ya Wakenya wa matabaka yote wakiwemo viongozi na wataalamu kueleza hofu yao baada ya raia wa China kuwasili nchini majuzi kuripotiwa kuugua.
Ilibidi Wakenya kuomba mahakama kushinikiz serikali kusimamisha safari zote za ndege kwenda na kutoka China.
Katika mtaa wa Sidai mjini Athir River, Kaunti ya Machakos, wakazi walilalamika baada ya Wachina kadhaa kuonekana wakiwa wamevaa vitambaa (barakoa) vya kufunika midomo na pua zao na ikaripotiwa kuwa baadhi yao walikuwa wagonjwa. Katika nyumba moja mtaani humo, raia mmoja wa China aliyekuwa miongoni mwa 239 waliowasili nchini Jumatano kwa ndege ya Shirika la China Southern Airline kutoka Guangzhuo, aliripotiwa kuwa hali mahututi. Maafisa wa polisi na madaktari walitumwa katika nyumba hiyo kukagua raia hao.
Katika Kaunti ya Kitui, wakazi walisema wanahofia afya zao baada ya raia sita wa China ambao wanafanya kazi katika kampuni ya ujenzi ya Sino Hydro Construction Company (SHCC) kuendelea kuzuiliwa katika kambi yao eneo la Mutomo, siku 10 baada ya kuwasili nchini.
Sita hao wametengwa ili kubaini ikiwa wana virusi vya Corona.
Wageni hao hawaruhusiwi kutangamanA na mtu yeyote na hali yao ya kiafya inafuatiliwa kila siku na maafisa wa serikali ya Kaunti ya Kitui wakiongozwa na Dkt Paul Kibati.
Hofu ya wakazi imesababishwa na ongezeko la idadi ya raia wa China wanaoshiriki katika ujenzi wa barabara ya Kibwezi- Kitui na bwawa la Thwake ambalo liko kati ya kaunti za Kitui na Makueni.
Katika Kaunti ya Narok, wakazi walieleza hofu ya kuambukizwa Corona baada ya raia kadhaa wa China wanaofanya kazi katika mradi wa ujenzi wa reli kutengwa kwa siku 14.
Wakazi hao walisema kwamba raia hao waliwasili nchini Februari 22 kutoka China wakiwa wamefunika nyuso kwa vitambaa hivyo.
Hofu ya kusambaa kwa virusi hivyo nchini ilidhihirika Wakenya kadhaa waliposhtaki serikali Ijumaa wakitaka isimamishe safari za ndege kutoka China.
Mahakama iliagiza serikali kufuta safari zote za ndege na kuchukua hatua za kulinda Wakenya mipakani. Kufuatia hofu ya kuzuka kwa maradhi hayo yanayooenea kwa haraka, Rais Uhuru Kenyatta aliunda kamati ya mawaziri kushughulikia Corona kama suala la dharura ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Wakenya wamelindwa dhidi ya virusi hivyo.
Miongoni mwa majukumu ya kamati hiyo itakayosimamiwa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliyeapishwa Ijumaa, ni kuhakikisha kuwa kuna wodi za kutengwa kwa walio na virusi hivyo katika hospitali ya Mbagathi, Nairobi na katika hospitali zote za rufaa za kaunti.
“Kamati hii itashirikiana kuidhinisha na kuchunguza masharti ya kuingia nchini kwa watu au makundi ya watu wanaotoka au wanaoshukiwa kutoka maeneo yaliyoathiriwa na virusi hivyo,” akasema Rais Uhuru mnamo Ijumaa.
Muda mfupi baada ya Rais Kenyatta kutoa amri hiyo kupitia kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, aliagiza wizara ya Ulinzi kutuma madaktari wa kijeshi katika viwanja vyote vya ndege, vituo vya kuingia nchini mipakani ili kusaidia kukagua wageni wanaoingia nchini.
Aidha, Bw Kinyua aliagiza wizara ya uchukuzi kuharakisha kufuta safari za ndege za moja kwa moja kutoka China. Ingawa alisisitiza kuwa hakuna kisa cha maambukizi ya Corona nchini, Bw Kinyua aliagiza Wizara ya Afya kushirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuhakikisha kuwa kuna wataalamu wa kutosha nchini kukabiliana na maradhi hayo.