Habari

Hospitali ya rufaa ya KU kufunguliwa rasmi Agosti

May 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

HOSPITALI Kuu ya Kenyatta University Referral Hospital, inatarajia kufungua milango yake rasmi Agosti, 2019.

Mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo Bi Olive Mugenda, amesema hospitali hiyo iligharimu takribani Sh8.7 bilioni ambapo ilijengwa na Wachina kwa zaidi ya miaka mitatu.

Tayari wajenzi hao wamekabidhi mamlaka yote kwa bodi ya hospitali hiyo inayosimamiwa na serikali.

Hafla hiyo ya kukabidhi bodi hiyo funguo za milango yote ya hospitali hiyo ilifanyika Ijumaa ambapo makundi mawili yalitia saini mkataba wa makubaliano na jinsi ujenzi huo ulivyotekelezwa.

“Tumefurahi kukabidhiwa funguo zote za hospitali hii na pia tayari tumetia saini makubaliano kati yetu sisi kama bodi ya hospitali na wajenzi kutoka China,” alisema Bi Mugenda.

 

Hospitali ya Kenyatta University Referral Hospital kufunguliwa rasmi Agosti 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

 

Alisema imechukua miaka  kumi wakitamani kuwa na hospitali ya  kimataifa na dakika za mwisho  maono hayo yametimia.

“Hospitali hii ni ya kimataifa na litashughulikia  magonjwa sugu kama lile la kitaifa la Kenyatta. Baada ya hospitali hiyo  kufunguliwa rasmi tunatumaini ya kwamba watu wengi hawatasafiri nchi za nje kama India na Ulaya kutafuta matibabu huko,” alisema Bi Mugenda.

Alisema wanataka kushirikiana na wataalam wa kiafya ili  kuweka kitengo cha kupambana na  saratani ya matiti ambayo imekuwa kero sana katika  nchi yetu.

Wahandisi wa kutoka China watia saini makubaliano baina yao na bodi ya hospitali ya Chuo Kikuu cha Kenyatta; Kenyatta University Hospital mnamo Ijumaa, Mei 24, 2019. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tutafanya juhudi kuona ya kwamba tunaajiri madaktari wenye ujuzi wa hali ya juu ili kukabiliana na maradhi sugu yanayosumbua wagonjwa wengi hapa nchini,” alisema Bi Mugenda.

Alizidi kueleza ya kwamba Juni watazingatia kuajiri wataalamu katika taaluma za juu kama madaktari na wakuu wa vitengo mbalimbali ambapo hivi karibuni watatangaza rasmi kwenye magazeti nafasi za kazi na “tutawaomba watu watume vyeti vyao vya masomo rasmi ili vichunguzwe kabla ya kuwaita kwa mahojiano zaidi.”

“Baada ya kukamilisha mipango hiyo, Julai tutaingilia mpango wa kuajiri kikundi kingine cha wataalamu kama wahasibu, na vyeo vingine muhimu vinavyohitajika,” alifafanua Mugenda.

Alisema hospitali hiyo itakuwa ni ya kipekee ambapo hata wagonjwa wengine “watazuru hapa kutoka nchi zingine.”

Wakati wa hafla hiyo Bi Mugenda aliandama na kamati kuu ya bodi ya hospitali hiyo, wahandisi wakuu wa kutoka China walioshuhudia ujenzi wa hospitali hiyo na wakuu wa kitengo cha afya katika hospitali hiyo.