Habari

Hospitali ya rufaa ya KU kufunguliwa rasmi Jumatatu

October 26th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

BAADA ya muda mrefu kabla ya kufungua milango yake, sasa ni rasmi kuwa hospitali kuu ya rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta itapokea wagonjwa kuanzia Oktoba 28, 2019.

Waziri wa Afya Bi Sicily Kariuki, alisema Ijumaa kwamba hospitali hiyo ya kisasa itakuwa na vitanda 650.

Hata hivyo aliongeza ya kwamba hospitali hiyo itaanza kwa kutumia vitanda 150 ambavyo vitatengwa kwa wagonjwa wenye maradhi ya saratani na matatizo ya figo.

“Nimeridhishwa na na vifaa vya kisasa vilivyoko hapa na baada ya wiki moja hali itakuwa shwari kwa sababu kazi itaendelea kama kawaida,” alisema Bi Kariuki.

Aliongeza kuwa ana imani ya kwamba hospitali hiyo itahudumia wagonjwa wengi kama Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).

Wakati wa ziara hiyo, waziri huyo aliandamana na mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo Bi Olive Mugenda na mkurugenzi wake Bw Andrew Toro.

Aidha, alisema hospitali hiyo itahudumia wagonjwa kwa asilimia 100 huku ikiwa na madaktari 40 waliohitimu pamoja na wauguzi kadha.

Waziri alisema alisema kitengo cha kutibu maradhi ya figo kitaendeshwa kwa asilimia 50.

Mwenyekiti wa bodi ya hospitali hiyo, Prof Olive Mugenda, alisema sasa kila kitu kipo shwari na wanangoja ifunguliwe rasmi ili wagonjwa waanze kutibiwa.

“Kuhusu uedeshaji wa hospitali hii, wasimamizi wake wameteuliwa tayari na kazi itaendeshwa kwa uwazi,” alisema Prof Mugenda.

Alifafanua na kusema ya kwamba hospitali hiyo itakuwa chini ya Wizara ya Afya kufuatia notisi ya gazeti rasmi la serikali.

Bi Mugenda aliomba radhi kwa kucheleweshwa kwa ufunguzi wa hospitali hiyo ambapo ilitarajiwa kufunguliwa Agosti mwaka huku wa 2019.

“Kulikuwepo na mipango ya kufanya majaribio ya vifaa hivyo na kuhakikisha viko sawa,” alisema Prof Mugenda.

Alisema hospitali hiyo inatarajiwa kufunguliwa Jumatatu na Rais Uhuru Kenyatta ili kuanza kazi rasmi.

Mnamo mwezi Juni 2019 waziri Kariuki na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha walizuru hospitali hiyo ili kujionea vifaa vipya vilivyowekwa vya kutumiwa huko.

Prof Magoha alitaja hospitali hiyo kama mojawapo ya kutambulika katika bara la Afrika.

Alisema baadhi ya vifaa vilivyoko katika hospitali hiyo utavipata katika hospitali za kimataifa na hata Afrika Kusini.