HUDUMA NAMBA: Sababu ya Wakenya kujikokota kujisajili
Na PETER MBURU
WAKENYA wengi wangali na wasiwasi kuhusu usalama wa habari zao za kibinafsi zinazohifadhiwa na serikali na mashirika ya kibinafsi.
Hofu hiyo imeripotiwa wakati serikali inaendeleza usajili wa habari hizo kidijitali kwa Huduma Namba huku wengi wakisusia zoezi hilo.
Licha ya kuwa serikali imekuwa ikitetea zoezi hilo kuwa halitakuwa na mwanya wa habari za Wakenya za kibinafsi kutumiwa isivyofaa, wengi wakiwemo viongozi bado hawajaridhishwa na maelezo yake.
Seneta wa Baringo, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Seneti Kuhusu Habari na Mawasiliano (ICT), Gideon Moi Jumatano alifichua kuwa pia yeye hajajisajili kwa Huduma Namba kutokana na hofu kuhusu usalama wa habari zake.
“Wakenya wanataka kuhakikishiwa kuwa habari zao zinalindwa. Hata mimi bado sijakubali kujisajili kwa Huduma Namba kutokana na hofu hiyo,” akasema Bw Moi.
Seneta Moi ni mmoja tu wa mamilioni ya Wakenya ambao wamesusia zoezi hilo kwa hofu hizo, japo serikali inazidi kutetea kuwa hakuna habari zitakazotumiwa vibaya na kuridhisha bunge kwa maelezo.
Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano, Bw Joe Mucheru alieleza kamati hiyo inayoongozwa na Bw Moi, kuwa serikali imeweka mikakati yote kuhakikisha kuwa habari za watu za kibinafsi hazitatumiwa vibaya na aidha mashirika ya serikali ama ya kibinafsi.
Bw Mucheru alisema hayo alipofika mbele ya kamati hiyo kufafanua kuhusu marekebisho kwenye Mswada wa Sheria ya Kulinda Habari.
Alisema Serikali itahakikisha kuwa shirika lolote linalohifadhi habari za mtu hazitatumia habari hizo kuuzia kampuni za kibiashara ama kufichua historia yake ya kisiri, na kuwa mtu anaweza kupewa habari zake na mashirika hayo akizihitaji.
“Ikiwa kampuni inahifadhi habari za mtu, sharti ifanye hivyo kwa sababu kamili. Hatutaki kuona mtu anapoacha habari zake ziwe zikitumiwa na wafanyabiashara kumuuzia bidhaa, kutambua mambo yake kuhusu jinsia ama madeni,” akasema Bw Mucheru.
Alitetea mswada huo aidha kuwa ni sehemu ya maendeleo taifa linapolenga kujikuza kiteknolojia na kuvutia watu kutoka mataifa mengine.
“Watu wasiwe na wasiwasi kuhusu Huduma Namba kwani serikali italinda habari zao,” akasema.