Huzuni mwanafunzi akifa baada ya upepo kuangusha paa la darasa Nakuru
SHULE moja Kaunti ya Nakuru imegubikwa na wingu jeusi la ukiwa baada ya upepo kung’oa paa la shule Ijumaa iliyopita na kusababisha mauti ya mwanafunzi mmoja na majeraha kwa wengine 13.
Tukio hilo lilifanyika katika Akademia ya St Pascal, Mtaa wa Mzee wa Nyama, Kaunti Ndogo ya Nakuru Mashariki. Liliathiri madarasa manne ambapo Brianna Maggy ambaye alijiunga na shule hiyo wiki mbili zilizopita, aliaga dunia.
“Tumepokea habari za kusikitisha kutoka kwa mwalimu kuwa Brianna alijeruhiwa baada ya kuangukiwa na paa. Tulipoenda hospitalini, tulipata amefariki kutokana na majeraha,” akasema Shangaziye Brianna na mlezi wake Shyler Namenya.
Babake Philip Kitatu alisema Brianna alikuwa amejiunga na shule hiyo kiwango cha chekechea na ndio alikuwa anawazoea wanafunzi wenzake kabla ya tukio hilo la mauti.
“Ni vigumu sana kuhimili yaliyotokea kwa sababu alikuwa na afya nzuri na sasa hayupo nasi tena,” akasema babake.
Mary Waithira, mwalimu wa PPA na madarasa ya chekechea alisema wanafunzi walikuwa wakienda kulala baada ya chakula cha mchana paa hilo lilipoanguka.
Wazazi wao walikuwa wawachukue saa 10 jioni. Hata hivyo, upepo mkali ulivuma na kupita lakini wa pili ukawa mkali zaidi na kung’oa poa.
“Upepo wa pili ulipovuma, wanafunzi walipiga nduru kwa sababu waliangukiwa na sehemu ya ukuta. Tuliwakimbiza walioumia hospitalini na Brianna akafa akipokea matibabu,” akaongeza Bi Waithira.
Supritendanti wa kimatibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Nakuru Dkt James Waweru alithibitisha kuwa wanafunzi 14 walipata majeraha.
Baadhi walipata majeraha madogo na wakatibiwa kisha kuruhusiwa kuenda nyumbani nao wasichana wawili wakalazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi.
“Mtoto mmoja alifariki na wengine wawili bado wanaendelea kupata matibabu,” akasema Dkt Waweru.
Wazazi na wakazi sasa wanataka uchunguzi ufanywe kuhusu ujenzi wa madarasa na hatua za dharura za kuzuia matukio kama hayo kuchukuliwa.