Habari

Huzuni mwanafunzi wa Kidato cha 3 shuleni Kisii High akianguka na kufariki

Na WYCLIFFE NYABERI January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

SIMANZI ilitanda katika Shule ya Wavulana ya Kisii Jumatano baada ya mwanafunzi wa Kidato cha Tatu kufariki baada ya kuanguka darasani.

Onesmas Raini, 16, alithibitishwa kufariki muda mfupi tu baada ya kukimbizwa katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Kisii (Ktrh) kupata matibabu baada ya kupoteza fahamu.

Kulingana na dadake Onesmas, Dorcah Bosibori, walipokea simu kutoka kwa shule hiyo Jumanne usiku na kuwafahamisha kwamba jamaa wao alikuwa amepelekwa hospitalini baada ya kuhisi vibaya wakiwa darasani.

Mara moja waliondoka nyumbani kuelekea hospitali na walipofika, walikuta mwili wake ukiwa kwenye eneo la dharura ukiwa umefunikwa kitambaa.

“Alithibitishwa kuwa amefariki na walikuwa wakitusubiri kabla ya kubeba mwili wake hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema binti huyo.

Bosibori aliongeza kuwa marehemu alimpigia simu wiki moja iliyopita, Januari 22, 2026 na kumwomba pesa kiasi.

“Nilimuuliza ikiwa alikuwa amemaliza pesa zake zote za mfukoni ambazo mama yangu alikuwa amempa. Aliniambia ndiyo. Bila kumwulizai zaidi, nilimtumia. Jana nilipata habari kuwa alikuwa mgonjwa hospitalini. Nilimwombea. Muda mfupi baadaye, nilipokea simu nyingine kwamba alikuwa amefariki,” Bi Bosibori alisema huku akibubujikwa na machozi nje ya chumba cha kuhifadhi maiti cha KTRH walipoenda kutazama maiti yake Jumatano asubuhi.

Raini anasemekana kutoka katika familia isiyojiweza na mama yake ambaye ni mjane ndiye amekuwa alibeba mzigo wa kumsomesha peke yake.

Mama huyo alikuwa na tumaini kuu katika maisha ya mtoto wake.

Familia hiyo ilitoa wito kwa wahisani kuwasaidia kupanga mazishi ya wanaposubiri upasuaji wa maiti ili kubaini chanzo cha kifo chake.