Huzuni mwanaume akimuua mwenzake kwa deni la Sh50
WAKAZI wa kijiji cha Mutitu, Kaunti ya Kirinyaga wamezidiwa na simanzi baada ya mwanaume kudungwa kisu na rafikiye kuhusu deni la Sh50.
Marehemu Jacob Maina aliaga dunia papo hapo kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa Novemba 12, 2025 iliyopita nyakati za jioni.
Kwa mujibu wa walioshuhudia tukio hilo, Bw Maina aligombana na rafikiye kuhusu deni la Sh50.
Ugomvi huo uliishia vita ambapo rafikiye alichomoa kisu chake na kumdunga kifuani.
Bw Maina alianguka chini na kufariki papo hapo kutokana na kuvuja damu nyingi.
Baada ya uvamizi huo mshukiwa alitoroka na kujificha lakini baadaye akafurushwa na makachero waliomnyaka na kumfungia katika kituo cha polisi cha Kerugoya kuhojiwa.
Wakazi wanasema tukio hilo limewashangaza sana kwa sababu hawakufikiria lingeishia mauti.
“Bado tumeshtuka kwa sababu hatukifikiria maafa yangetokea kijijini hapa kutokana na deni la Sh50. Mshukiwa amemuua rafikiye mkubwa na anastahili kukabiliwa kisheria,” akasema Mary Wanjohi.
Kamanda wa Polisi wa Kirinyaga Nelson Taliti alisema suala hilo linashughulikiwa kama mauaji na akahakikishia familia iliyofiwa kuwa watapata haki.