Habari

Huzuni na lawama baada ya wanafunzi wa Dr Aggrey, Taita Taveta kufa ajalini

Na LUCY MKANYIKA February 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

FAMILIA za wanafunzi wanne wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Dr Aggrey waliokuwa kati ya watu sita waliofariki kwenye ajali Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta mnamo Jumamosi, zimeeleza masikitiko kuhusu jinsi watoto hao walivyopoteza maisha.

Baadhi ya familia zilisimulia jinsi walivyopokea mawasiliano kutoka kwa wanao kwamba shule ilifungwa baada ya kisa cha moto, na walihitaji kutumiwa nauli ya kurudi nyumbani.

Bw Randu Kombe, mzazi ambaye alimpoteza mtoto wake wa kidato cha pili, alisema wazazi hawakujulishwa kuhusu sababu za kufungwa kwa shule.

Kulingana naye, wasimamizi wa shule walikuwa na jukumu la kuwafahamisha wazazi kuhusu yale yaliyokuwa yakiendelea badala ya kuwaacha wanafunzi wenyewe kuanza kutafuta wazazi wao wakiomba nauli, na pia bila kuzingatia wakati ambao watoto wanaosafiri hadi mbali wangefika nyumbani.

Jumapili, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Robert Aran, alisema watashirikiana na familia zilizoathirika.

Huku akieleza masikitiko kuhusu ajali hiyo, Bw Aran alisema hawakuwa na budi ila kuwaruhusu watoto kurudi nyumbani ili kuzuia ghasia shuleni na uharibifu wa mali kufuatia kisa cha pili cha moto.

Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, alituma risala za rambirambi kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, kupitia taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari.

Kulingana na mashahidi, ajali hiyo ya Jumamosi jioni ilitokea wakati dereva wa gari aliposhindwa kulidhibiti barabarani.

Wanafunzi hao walikuwa wakirejea nyumbani baada ya shule hiyo kufungwa kwa muda usiojulikana mapema Jumamosi kufuatia tukio la moto.

Ilikuwa mara ya pili moto kutokea shuleni humo ndani ya siku chache.

Basi walilokuwa wakisafiria lilikuwa likielekea Voi ajali ilipotokea. Dereva wa basi hilo, Martin Joseph, alisema gari halikuwa na hitilafu yoyote kabla kuanza safari ila walipokuwa njiani, breki ikapata hitilafu.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Taita Taveta, Ali Ndiema, alithibitisha kisa hicho na kusema uchunguzi ulianzishwa kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.

Viongozi wa kisiasa na wa kidini walitoa wito kwa Mamlaka ya Barabara za Kitaifa nchini (KENHA) izingatie kubadilisha muundo wa barabara hiyo katika sehemu ya Josa ili kuepusha ajali za mara kwa mara.