Huzuni vijana tisa wakiuawa na pombe haramu
VIJANA tisa wamepoteza maisha mwaka huu kutokana na pombe haramu katika Wadi ya Kabiria na maeneo jirani ya Dagoretti Kusini, kaunti ya Nairobi.
Matukio haya yametokana na ongezeko la baa na maduka yasiyo na leseni, yaliyoenea ndani ya ploti za makazi, yakihatarisha maisha na kuvunja familia.
Novemba 10, 2025, wakazi waliandamana barabarani wakitaka serikali ichukue hatua.
Walidia kuna ushirikiano kati ya baadhi ya maafisa wa polisi na wauzaji wa pombe haramu.
Walidai kwamba vijana watatu walifariki wiki hii kutokana na pombe haramu
“Mwanaume mmoja alitutisha akiwa na panga, na polisi waliondoka bila kuchukua hatua,” alisema mama mmoja aliyepoteza mtoto wake. Wanawake hao waliapa kuendelea na harakati zao hadi kila baa haramu katika Kabiria, Adonai, Stage 2 na maeneo yote ya Dagoretti Kusini ifungwe.
Akizungumza na Taifa Leo, Afisa Mkuu wa Mazingira wa Kaunti ya Nairobi, Bw Geoffrey Mosiria Mosiria alifichua kuwa vijana tisa wamefariki baada ya kunywa pombe hatari mwaka huu.
Baada ya maandamano,alifika eneo hilo na kuahidi hatua kali. “Serikali ya Kaunti haitavumilia baa zisizo na leseni wala pombe zisizo salama,” alisema Mosiria. Aliongeza kuwa kikosi cha Idara tofauti kitaendesha oparesheni wiki hii, kwa lengo la kufunga baa zote zisizo na leseni, hasa zile zilizo ndani ya ploti za makazi.
Mosiria alifichua kuwa kati ya vijana waliopoteza maisha mwaka huu, wawili wanatarajiwa kuzikwa wiki hii kutokana na pombe hatari. “Operesheni haitakuwa kama kawaida,” alisema, “nimezindua vita dhidi ya pombe haramu na baa zisizo na leseni.”