Habari

Huzuni watu wanane wakifa ajalini Nyamira usiku wa kuamkia Jumapili

Na RUTH MBULA December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WIMBI la huzuni Jumapili, Desemba 14, 2025 liligubika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyamira wakati ambapo familia waliopoteza jamaa zao kwenye ajali walifika kutazama miili.

Ajali hiyo iliyotokea kwenye barabara ya Bwárani-Tombe katika barabara ya Kericho-Nyamira ilisababisha mauti ya watu wanane.

Kati ya miili hiyo minane, wawili walikuwa watoto wa chini ya umri wa miaka miwili. Uchungu zaidi ni kwamba miili yao ililala kwenye vifua vya mama yao.

Jones Kebaso alisema jamaa zake wanne walihusika kwenye ajali hiyo ya saa mbili usiku wa kuamkia Jumapili.

Alifiwa na mpwa wake pamoja na shemejiye.

Jamaa zake wengine wawili wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyamira wakiwa katika hali mbaya kiafya. Baadhi wana majeraha mabaya ya kichwa na wapo katika chumba cha wagonjwa mahututi.

“Tunaendelea kufanya maandalizi wahamishwe hadi Eldoret. Walikuwa wakitoka Nairobi wakija nyumbani Kenyenya, Nyamira Kusini kwa mazishi ya mjomba wetu,” akasema Bw Kebaso.

“Mjomba wetu amekuwa akiugua kwa miaka tisa lakini akaaga na tulikuwa tunajiandaa kwa mazishi yake. Sasa tuna jamaa zetu wawili zaidi wameaga na wengine wawili wakiwa mahututi,” akaongeza.

Mabaki ya matatu ya kampuni ya Quarser Sacco iliyohusika kwenye ajali mbaya katika barabara ya Kericho-Nyamira Jumamosi usiku. Picha|Ruth Mbula

Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu Nyamira Jared Oeba alithibitisha kuwa watu wanane waliaga dunia kwenye ajali hiyo.

Wengine saba walinusurika na wakakimbizwa hospitalini huku wanne wakipambana kusalia hai katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Polisi wanasema ajali hiyo ilihusisha trela KBE 701E ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyetoweka baada ya ajali hiyo.

Trela hilo liligongana na gari aina ya Nissan KCF O68V ambalo ni la Quarser Sacco. Dereva wa Nissan aliaga dunia papo hapo.

“Trela lilikuwa likiendeshwa kuelekea Kericho na lilipofika eneo la ajali, dereva alishindwa kulidhibiti ndiposa likagongana na matatu iliyokuwa ikielekea Nyamira,” ikasema ripoti ya polisi.

Katika eneo la tukio, umati ulijawa na jazba na ukaanza kufyonza mafuta kutoka trela kisha kuwapora wafu na walionusurika kwenye ajali.

Umati huo ulionyesha ukatili zaidi baada ya kuwarushia mawe polisi waliowafurusha.

“Mmoja wa afisa wetu alifyatua risasi mara tano hewani kufukuza umati huo,” ikasema taarifa ya polisi.

Magari hayo mawili yalikokotwa hadi kituo cha polisi cha Nyamira kufanyiwa ukaguzi.

Beatrice Arani ambaye alishuhudia ajali hiyo ikitokea, alisema eneo la Bwárani limekuwa hatari zaidi kutokana na visa vya mara kwa mara vya ajali.

“Tunaomba serikali ione mbinu itakayotumia kuepuka ajali zaidi katika barabara hii,” akasema Bi Arani.

Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo ambaye aliwatembelea manusura hospitali, alisema kaunti inaendeleza mipango kuhakikisha kwamba wagonjwa wawili mahututi wanahamishwa kwa matibabu spesheli.

“Wanahitaji upasuaji kwa sababu wana majeraha mabaya kichwani,” akasema Bw Nyaribo.

Gavana huyo alienda katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo aliwafariji jamaa na marafiki.

“Tumeanzisha kamati kufahamu jinsi tutakavyosaidia familia zilizoathirika,” akasema Bw Nyaribo.