Ichungwah akerwa na Ruto, asema anaweza kutimuliwa na Bunge
SAA chache tu baada ya Rais William Ruto kuzindua kundi la kupambana na ufisadi uliokita mizizi katika sekta ya umma, huku akiendeleza lawama zake za hongo Bungeni, wabunge walijibu kwa hasira, wakimtaja Rais kama mshiriki mkuu wa sakata kubwa za ufisadi.
Kwa mara ya tatu, katika mkutano wa Kundi la Bunge la Kenya Kwanza na ODM uliofanyika Agosti 18, 2025, Rais Ruto aliwashutumu wabunge kwa kushiriki katika ufisadi kwa kudai hongo ili kuuliza maswali, kuwasilisha hoja, kubadilisha miswada, au kutoa ripoti nzuri kwa wale wanaofika mbele ya kamati za bunge.
Hata hivyo, wabunge wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah (Kikuyu) na mwenzake wa wachache Junet Mohamed (Suna Mashariki), wakionekana kuchoshwa na kile walichokitaja kama kudhalilishwa na Ikulu, walijibu vikali katika kikao cha alasiri, wakisema kuwa serikali kuu inapoteza mwelekeo.
“Tuna wanaume na wanawake waliochaguliwa na wananchi kuwakilisha masilahi yao na kusimamia serikali kwa niaba yao,” alisema Bw Ichung’wah.
“Tunaposimamia serikali, hatufanyi hivyo kwa upendeleo. Sio kwa niaba ya Rais wala Mahakama,” aliongeza, huku akiwaomba wabunge wasitishwe na kauli za Rais.
“Bunge hili lina mamlaka ya kumuondoa yeyote serikalini, lakini hakuna yeyote serikalini anayeweza kuwaondoa ninyi. Nimeumizwa sana na tuhuma hizi za ufisadi,” alisema Ichung’wah.
Kwa upande wake, Bw Junet alisema: “Nimesema kwenye Bunge hili awali kuwa watu huchukulia nafasi ya ubunge kama mzaha. Lakini wakijaribu kugombea, watajua ilivyo vigumu.”
“Haiwezekani kuchafua Bunge lote kwa ujumla. Kama una tatizo na mtu binafsi, sema. Bunge hili ndilo lenye mamlaka ya moja kwa moja kuwakilisha maslahi ya wananchi,” aliongeza.
Mbunge wa Tharaka, Gitonga Murugara, ambaye aliwasilisha hoja ya dharura kuijadili sakata ya hongo bungeni, alimshauri Rais Ruto “aseme ni mbunge gani au ni wabunge gani waliodai au waliopokea Sh150 milioni au hongo yoyote ile.”
Rais alidai katika mkutano wa kundi la wabunge kwamba baadhi ya wabunge wamekuwa wakidai hadi Sh150 milioni kutoka kwa watu wanaofika mbele yao, akidai ni fedha za serikali za kaunti.
Lakini Bw Murugara alimtaka Rais awasilishe ushahidi wake kwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ili uchunguzi ufanyike.
Kupitia Amri ya Rais ya Kwanza mwaka 2025, Rais Ruto alianzisha rasmi jopo kazi la mashirika mbali mbali chini ya Idara ya Haki, Haki za Kibinadamu na Masuala ya Katiba, akiunganisha taasisi za serikali zinazohusika na uchunguzi na uangalizi wa masuala ya ufisadi.
Taasisi hizo ni pamoja na Afisi ya Rais itakayoongoza kikosi hicho, Mwanasheria Mkuu ambaye atakuwa katibu, Idara ya Ujasusi wa Kitaifa (NIS), EACC, Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), Kituo cha Kuripoti Fedha (FRC), Shirika la Kutwaa Mali (ARA), Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), Benki Kuu ya Kenya (CBK), na Mamlaka ya Kusimamia Ununuzi wa Umma (PPRA).
Mbunge wa Rarieda, Otiende Amollo, alisema hajawahi kutafuta wala kupokea hongo yoyote.
“Rais alipaswa kuandika ujumbe rasmi kwa Spika kuhusu madai anayotoa ili uwasilishwe. Sio kutuonyesha kama wahalifu. Hii ni fedheha. Tumia mamlaka yako kuagiza Kamati ya Madaraka na Haki za Bunge kumwita Rais, au mkuu wa utumishi wa umma, waje watuambie nani alipokea hizo hongo,” alisema Dkt Amollo.
Mbunge wa Endebess, Dkt Robert Pukose, naye alisema “Ni aibu kubwa kwa Rais kusimama hadharani na kushutumu Bunge hili. Hili linapaswa kuchunguzwa na ukweli ujulikane. Wananchi sasa wanatuona kama wezi, ilhali tuna familia.”
Akijibu kwa ukali, Mbunge wa Tetu, Geoffrey Wandeto, alisema Bunge ni hekalu la demokrasia.
“Kile tumeshuhudia kwa wiki mbili zilizopita kinatia hofu. Serikali kuu imedai kuna ufisadi hapa bungeni. Tunahisi tuko hatarini hata mitaani,” alisema Bw Wandeto.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bumula, Wamboka Wanami, alisema kuwa Bunge linashambuliwa kwa sababu limefichua walioshiriki katika sakata ya e-Citizen na jinsi fedha zinavyopotea kupitia jukwaa la kidijitali la ukusanyaji mapato.
“Ni makosa kwa Rais kusema anapewa taarifa za kijasusi halafu kutoa kauli nzito namna hiyo. Sheria inasema mtu yeyote anayejua uhalifu umetendeka na anakaa kimya, basi huyo naye ni mshirika. Katika hali hii, Rais naye ni mshirika,” alisema Bw Wanami.