IEBC yageukia data kusajili wapigakura wapya milioni 6 kufikia uchaguzi mkuu ujao
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imegeukia matumizi zaidi ya data ya kisayansi katika Taasisi ya Kitaifa ya Usajili (NRB) na Idara ya Huduma za Uhamiaji (DIS) kuweka malengo yake ya kusajili wapigakura huku ikisaka usahihi kwenye sajili yake.
Awali, IEBC iliegemea mfumo wa zamani wa sensa kuweka malengo yake ya kusajili wapigakura, ambao, inasema sasa “umethibitisha kukosa usahihi, ustawishaji na siyo halisi.”
Hata hivyo, huku tume hiyo ya uchaguzi ikitangaza mageuzi hayo katika ripoti iliyowasilishwa na Kamati ya Uangalizi kuhusu Utekelezaji wa Katiba (CIOC) ya Bunge la Kitaifa, ingali na matumaini ya kufanikisha wapigakura wapya milioni 6.3 kabla ya uchaguzi mkuu 2027.
Shabaha ya wapigakura wapya milioni 6.3iliwekwa kwa kutumia mfumo wa data ya sensa uliotegemea watu Waliohitimu Umri wa Kupiga kura (VAP), ambao tume sasa inautema na kuegemea “data iliyo sahihi zaidi ya NRB na DIS” inayojikita kwenye Watu Wanaohitimu kuwa Wapigakura (VEP).
“Tume iliashiria inahamisha mchakato wa kupanga malengo yake kutoka VAP hadi VEP, inayozingatia zaidi idadi halisi ya wananchi wanaomiliki stakabadhi zinazohitajika za usajili,” inaeleza ripoti ya CIOC, ambayo mwenyekiti wake ni Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi.
Katiba kwenye Kifungu 83 inaeleza masharti yanayohitaji kutimizwa ili kusajiliwa kama mpigakura, ambapo matakwa ya kisheria yanajumuisha kumiliki kitambulisho cha kitaifa au pasipoti halisi ya Kenya.
Endapo tume itafanikisha kusajili wapigakura wapya 6.3 milioni, wapiga kura waliosajiliwa katika uchaguzi mkuu wa 2027 watafikia 28.4 milioni ikilinganishwa na wapigakura 22.1 milioni walioidhinishwa kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.
“Tume ilibaini kuwa mfumo wa VEP unatumia data kutoka NRB na DIS, hivyo basi kupunguza malengo yanayopangwa kutokana na vitambulisho na pasipoti zilizotolewa,” ilisema CIOC.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa “mwelekeo huu wa malengo yanayoendeswa na data inayotokana na idadi halisi ya vitambulisho vya kitaifa na pasipoti unahakikisha rasilimali zinagawanywa ipasavyo na vigezo vya utendakazi ni vya kihalisia na vinavyoweza kutimizwa”.
Tume imekuwa ikitumia data ya sensa kuainisha raia waliohitimu na kukadiria malengo ya usajili wa wapigakura kwa kuhesabu idadi ya watu watakaokuwa wamehitimu umri wa miaka 18 kufikia uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, tume inasema muundo wa ripoti ya sensa unajumuisha watu ambao hawajahitimu kusajiliwa kama wapigakura.
Hii inajumuisha watu wasio raia, ambao hawajaandikishwa na wakimbizi, “na kusababisha ongezeko la shabaha isiyooana na data kwa misingi ya sheria.”
Kuhusu usajili wa wapigakura, tume ya uchaguzi ilisema ili kufanikisha malengo ya kusajili wapiga kura na kuhakikisha “hakuna Mkenya anayenyimwa haki ya kupiga kura,” inanuia kutumia “mikakati kadhaa” ikiwemo shughuli endelevu ya kusajili wapigakura katika kila moja ya afisi 290 za IEBC kwenye maeneobunge.