IEBC yahimiza amani DCP ikilalama Magarini
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), imewataka wanasiasa kuelekeza nguvu zao katika kuhimiza amani na utulivu, badala ya kutoa matamshi yanayoweza kuchochea taharuki miongoni mwa wananchi.
Kamishna wa IEBC, Dkt Alutalala Mukhwana, alisema baadhi ya matamshi yanayotolewa na viongozi wa kisiasa, hasa yanayoonesha shaka kuhusu uwezo wa IEBC kusimamia uchaguzi huru na wa haki, yanaweza kuathiri mtazamo wa umma na kuzua hali ya kutoaminiana bila sababu.
Alikuwa akizungumza katika kikao na wanahabari mjini Hola, Kaunti ya Tana River Novemba 23, 2025 ikiwa siku ya mwisho ya kampeni za chaguzi ndogo zitakazofanyika maeneo tofauti nchini Novemba 27, 2025.
“Kila maoni ya kutilia shaka taasisi ya uchaguzi yanaathiri wananchi moja kwa moja. Tunawaomba wanasiasa kupunguza joto la kisiasa na kuanza kuhubiri amani,” alisema.
Matamshi yake yalitokea wakati ambapo Chama cha DCP kikiongozwa na aliyekuwa naibu rais, Bw Rigathi Gachagua, kimeibua madai kuhusu ukosefu wa uaminifu katika uchaguzi mdogo wa Magarini.
Uchaguzi huo ulio na wagombeaji 10 umevutia ushindani mkali kati ya Bw Harrison Kombe wa Chama cha ODM, na Bw Stanley Kenga wa DCP.
Hata hivyo, Gavana wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, alipuuzilia mbali madai ya Bw Gachagua, akisema hizo ni dalili za kuashiria DCP wameona wanaelekea kushindwa uchaguzini.
Dkt Mukhwana alisisitiza kuwa IEBC imekamilisha maandalizi yote muhimu kuhakikisha kwamba chaguzi ndogo zinakuwa za kuigwa, na kwamba zitatoa mwelekeo wa namna uchaguzi mkuu wa 2027 utakavyotekelezwa.
Aliahidi kuwa Tume itahakikisha uwazi, uadilifu na kuzingatia sheria katika kila hatua ya mchakato wa upigaji kura.
“Tume imejipanga kikamilifu. Tunataka uchaguzi huu uwe mfano wa kuigwa. Tunaomba viongozi wasiwe chanzo cha hofu kwa wananchi,” aliongeza.
Aidha, kamishna huyo aliwakumbusha wanasiasa kuwa katika kila kinyang’anyiro cha kidemokrasia, lazima kuwe na mshindi na pia mshinde, akiwashauri kuanza kujitayarisha kwa matokeo yoyote badala ya kuchochea hisia kali.
Alisema mchakato wa uchaguzi haupaswi kugeuzwa chanzo cha migogoro au mgawanyiko wa kijamii, hususan katika maeneo yanayotajwa kuwa na ushindani mkali.