IG Kanja, Tume ya polisi wapigania udhibiti wa shughuli ya kusajili makurutu 10,000
VITA vya ubabe kati ya Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na baadhi ya makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Polisi (NPSC) huenda vikasambaratisha shughuli ya usajili wa makurutu wapya 10,000 wa polisi mwezi ujao, Septemba.
Mvutano huo umegawanya tume hiyo, ambayo Bw Kanja ni mwanachama wake, katika makundi mawili.
Kundi moja ni la makamishna ambao ni maafisa wa polisi, wakiongozwa na Bw Kanja mwenyewe, huku kundi jingine likishirikisha makamishna raia likijumuisha mwenyekiti wa NPSC.
Mwenyekiti huyo anashikilia kuwa majukumu yote kuhusu maafisa wa polisi, ikwemo bajeti ya Sh60 bilioni ya mishahara yao, uajiri, upandishaji vyeo na uhamisho yanapaswa kusimamiwa na NPSC.
Kiini cha mvutano huo ni shughuli ijayo ya usajili wa makurutu wapya 10,000 ambayo tume hiyo inapendekeza iendeshwe kwa mfumo mpya wa kidijitali.
Taifa Leo imegundua kuwa mbinu hiyo mpya ya usajili imevutia hisia za Baraza la Kitaifa la Usalama (NSC) linaloongozwa na Rais William Ruto.

Jana, tume ya NPSC ilianzisha mchakato wa kitaifa wa ukusanyaji maoni kuhusu mfumo huo mpya uliopendekezwa kutumika kuendeshea usajili wa makurutu wapya wa polisi.
Hii ni licha ya kwamba baraza la NSC limetoa ushauri kwamba utekelezaji wa mfumo huo usitumike katika shughuli ya mwezi ujao.
Imeripotiwa kuwa baraza hilo la usalama limeshauri kwamba shughuli hiyo iendeshwe kwa njia ya zamani ambapo vijana wanajitokeza katika vituo mbalimbali kufanyiwa majaribio.
Kutokana na mgawanyiko katika NPSC, Rais William Ruto au Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen watahitaji kuingilia kati ili kufanikisha kuendeshwa kwa zoezi hilo muhimu.
NPSC imealika umma kuwasilisha memoranda, zilizoandikwa au kutolewa kwa midomo, kuhusu kanuni hiyo iliyopendekezwa kutumika katika usajili huo.
Kulingana na kanuni hiyo, ni lazima kwa wanaopata kusajiliwa kwa mafunzo ya kuwa polisi kuwasilisha maombi kwa njia ya mtandao. Baada ya hapo wataorodheshwa na kualikwa katika vituo vya usajli kufanyiwa usaili wa kimwili.