Jacque Maribe na mchumba wake waanza safari ya kujinasua
Na Richard Munguti
MTANGAZAJI wa runinga Jacque Maribe na mchumba wake Jumatatu walikanusha shtaka la kumuua mfanyabiashara Monica Nyawira Kimani.
Kushtakiwa kwa wapenzi hawa Maribe na Joseph Irungu almaarufu Jowi kulifuatia kibali cha mtaalamu wa tiba ya maradhi ya wenda-wazimu hospitalini Mathari, Nairobi aliyetoa ripoti kuwa “wote walikuwa na akili timamu. Wanaweza kujibu shtaka.”
Wiki iliyopita wawili hao hawangeweza kujibu shtaka kwa kuwa Bi Maribe hakuwa amepimwa akili licha ya kukaa rumande kwa siku 10 akiendelea kuhojiwa na maafisa wa polisi kuhusu mauaji ya Monica.
Monica aliuawa ndani ya nyumba yake mtaani Kilimani aliporejea nchini kutoka Sudan Kusini alikokuwa anafanya biashara. Mawakili Katwa Kigen na Dunstan Omar wanaomwakilisha Bi Maribe waliomba aachiliwe kwa dhamana wakisema “amekuwa ndani kwa siku 15 sasa na anapaswa kuachiliwa huru kwa dhamana”.
Bw Kigen alieleza korti kuwa walimkabidhi kiongozi wa mashtaka Bi Catherine Mwaniki nakala za ombi lao la dhamana ya Bi Maribe lakini hawajapata majibu.
“Naomba mahakama iamuru Bi Mwaniki ajibu ombi la kuachiliwa kwa dhamana kwa Bi Maribe. Naomba mahakama imwagize aseme ikiwa anapinga ombi hili au la,” alisema Bw Kigen.
Bw Mwaniki aliambia mahakama kuwa ameagizwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji aombe washtakiwa wazuiliwe kwa wiki mbili ili polisi wakamilishe uchunguzi.
Aliongeza kusema kuwa afisa anayechunguza kesi hiyo amewasilisha ushahidi wake katika ombi hilo la kuachiliwa kwa dhamana.
Katika ombi lake, Bi Maribe anasema kuwa dhamana ni haki ya kila mshukiwa kwa mujibu wa kifungu 49 cha katiba.
Bi Maribe alisema ameshirikiana na maafisa wa polisi wanaochunguza kesi dhidi yake. Aliongeza kuwa atafika mahakamani wakati wowote ule anapotakiwa na “kuwa atawasilisha pasi yake ya kusafiri mahakamani.”
Mshtakiwa ameahidi kutii masharti atakayopewa na mahakama.
Bw Irungu almaarufu Jowi pia ameomba korti imwachilie kwa dhamana kupitia kwa wakili Cliff Ombeta.
Bi Mwaniki alimweleza Jaji Jessie Lesiit kuwa upande wa mashtaka unapinga vikali washtakiwa kuachiliwa kwa dhamana kwa kuwa adhabu kali inawasubiri washtakiwa hawa wakipatikana na hatia.
“Washtakiwa hawawezi kuaminika endapo watarudi tena mahakamani kuendelea na kesi,” alisema afisa anayechunguza kesi hiyo.
Na wakati huo huo wakili anayewakilisha familia ya Monica, Bw Herman Owili alimweleza Jaji Lesiit kuwa ameombwa aeleze korti isiwaachilie wapenzi hao kwa dhamana.
Bw Owili aliambia mahakama atawasilisha sababu za kupinga wakili hao wakiachiliwa kwa dhamana. Jaji Lesiit alimwagiza wakili wa familia awakabidhi Mabw Kigen na Ombeta nakala za ombi lake ndipo wawasilishe majibu kabla ya Jumatano kesi itakapowasilishwa mbele ya Jaji James Wakiaga.
Jaji huyo aliwataka mawakili hao wamweleza Jaji Wakiaga sababu za kutaka washtakiwa hao waachiliwe kwa dhamana.
Mwili wa Monica ulikutwa kwenye bafu ukielea majini baada ya kukatwa shingo huku amefungwa mikono.
Jowi alitiwa nguvuni mnamo Septemba 25 siku nne baada ya mwili wa Monica kupatikana nyumbani kwake.
Jaji Lesiit aliamuru washtakiwa wazuiliwe hadi kesho Jumatano mbele ya Jaji Wakiaga ndipo wawasilishe ombi la kuachiliwa kwa dhamana.
Bw Irungu anauguza jeraha la kupigwa risasi kwenye bega la mkono.
Anaomba aachiliwe kwa dhamana aende hospitali. Kesi itatajwa Alhamisi.