Habari

Jaguar kulala seli kwa siku ya pili

June 27th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Starehe Charles Njagua atalala kwa mara nyingine katika seli za kituo cha polisi baada ya mahakama kuomba ipewe muda wa kuchunguza ombi lake la kutaka aachiliwe kwa dhamana.

Upande wa mashtaka hata hivyo unataka mbunge huyo azuiliwe kwa siku 14 zaidi ili wapelelezi wapate nafasi ya kukamilisha uchunguzi kuhusu madai eti alitoa matamshi ya uchochezi dhidi ya wafanyabiashara raia wa kigeni walio nchini hususan katika jiji kuu la Nairobi.

Wakili wake Dancan Okach hata hivyo amepinga hatua ya kuhamishwa kwa mbunge huyo kutoka kituo cha polisi cha Kileleshwa hadi kile cha Kamukunji, akitaja hatua hiyo kama ukiukaji wa haki zake.

Bw Njagua, maarufu kama Jaguar, alikamatwa Jumatano na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) nje ya majengo ya Bunge.

Mbunge huyo anatuhumiwa kutoa matamshi ya uchochezi dhidi ya raia wa kigeni wanaoendesha biashara jijini Nairobi na kutaka wafurushwe nchini kwa nguvu.

Hata hivyo, mbunge huyo amedai kuwa madai yake yalitokana na malalamishi ya wafanyabiashara wenyeji kwamba wageni wameingilia biashara ndogondogo, yalifasiriwa visivyo.

“Matamshi yangu yalifasiriwa vibaya. Sikusema kwamba wageni wanaoendesha biashara halali nchini wavamiwe na kufurushwa. Sisi kama Wakenya tunapenda amani na hatungependa kuvuruga biashara zozote hata zile zinazoendeshwa na wageni,” akasema Jumatano asubuhi kwenye mahojiano katika runinga ya K24 akiwa nyumbani kwake.

Serikali ya Tanzania imelaani matamshi hayo ikidai yanaweza kusababisha kudhuriwa kwa raia wake wengi wanaoendesha biashara ndogondogo hasa katika soko maarufu la Gikomba, Nairobi.

Serikali ya Kenya pia imejitenga na matamshi hayo na kuwahikikishia wageni kuwa usalama wao utalindwa pamoja na mali yao.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya Habari Jumatano, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ilikashifu matamshi hayo ikisema ni kielelezo cha matumizi mabaya ya uhusu wa usemi hali inayohujumu sifa ya Kenya ya kuwavumilia wageni.