Jaji aamua hospitali hazifai kuzuilia maiti kwa sababu ya bili
HOSPITALI hazina haki ya kuzuilia maiti au kutumia mwili wa mtu kama dhamana hadi gharama ya matibabu itakapolipwa, mahakama imeamua.
Jaji wa Mahakama Kuu Nixon Sifuna alisema hakuna sheria inayoruhusu hospitali kuwa na haki kama hiyo kuhusu wagonjwa au mili yao iwapo wagonjwa hao wanakufa baada ya kulazwa au wakati wa matibabu.
“Hiki ni kitendo kisicho rasmi ambacho kimekuwa desturi na kutumiwa sana kiasi kwamba kinaonekana kuwa kitu halali, licha ya kutokuwa na msingi wa kisheria,” jaji alisema.
Akiagiza Hospitali ya Mater kutoa maiti ya Bi Caroline Nthangu Tito kwa familia yake kwa mazishi, Jaji Sifuna alisema madeni yanayohusiana na gharama za matibabu yanapaswa kudaiwa kama madeni ya kiraia na kufuatiliwa kwa njia hiyo.
Jaji huyo aliagiza hospitali kutoa maiti kwa mwana wa Bi Nthangu, Moses Mutua, na kusema mbali na gharama za kuhifadhi maiti, sehemu ya bili inayohusiana na matibabu na dawa ambayo familia haikupinga, inapaswa kufuatiliwa kama deni la kawaida na kwa njia halali za ukusanyaji wa madeni.
“Kwa hali hii, mahakama hii inabaini kwamba kuwekwa na kuendelea kuwekwa kwa mwili wa marehemu Caroline Nthangu Tito na Hospitali ya Mater ni kosa wala hakuna msingi wa kisheria,” alisema Jaji.
Mwanamke huyo alifariki hospitalini Agosti 2, 2025 akipata matibabu.
Bw Mutua alisema kabla ya mama yake kufariki, alikuwa na bili ya Sh3.3 milioni.
Hospitali ilikataa kutoa maiti hadi familia ilipe bili hiyo. Bw Mutua aliambia mahakama kuwa kuwekwa kwa maiti mochari kumewasababishia msongo wa mawazo kwa kuwa gharama ya kuhifadhi ilikuwa ikiongezeka kwa Sh2,000 kila siku.
Alisema yeye na kaka yake walikuwa wanafunzi wa chuo na hawakuwa na kipato cha kudumu, na kwamba walikuwa wakitegemea mama yao marehemu kwa msaada wa kifedha. Alisema baba yao, Tillers Mutua, alifariki mwaka 2023.
Alisema walikuwa tayari kwa makubaliano ya jinsi ya kulipa bili na hospitali lakini usimamizi wa hospitali ulikataa kushirikiana hadi walipe deni lote.
Alisema kuwekwa kwa maiti kumewasababishia huzuni kubwa na matatizo makubwa ya kifedha kutokana na kuongezeka kwa gharama za kuhifadhi maiti.
Katika uamuzi wake, Jaji Sifuna alisema mtu akifariki, maiti yake inapaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Umma na kanuni zake, mojawapo ikiwa ni kwamba maiti inapaswa kuzikwa.
“Kijamii, kuwekwa kwa maiti na hospitali au mochari kwa sababu ya deni, kunasababishia msongo wa mawazo familia zinazolia na pia ni ukatili kwa marehemu. Hali hii imekuwa ikitumiwa mara nyingi kuwatisha, kusababishia aibu, kuhangaisha na kushinikiza familia zinazolia ili zikubali mahitaji ya kifedha ya hospitali,” jaji alibainisha.