Jaji akataa ombi la Facebook kusitisha kesi waliyoshtakiwa na wadhibiti maudhui
JAJI amekataa kusitisha kesi iliyowasilishwa na wasimamizi wa maudhui 186 walioshtaki mmiliki wa Facebook, Meta Platforms, na maajenti wake, wakipinga kufutwa kazi.
Meta na mshirika wake Samasource Kenya EPZ walitaka kesi hiyo isitishwe hadi pale rufaa yao katika Mahakama ya Juu itakaposikilizwa, baada ya Mahakama ya Rufaa kutupilia mbali ombi lao la kupinga mahakama za Kenya kusikiliza kesi hiyo mnamo Septemba mwaka jana.
Hata hivyo, Jaji Nduma Nderi alisema mahakama yake haina uwezo wa kutathmini maamuzi ya Mahakama ya Rufaa ili kuamua iwapo kesi hiyo inaweza kusitishwa.
“Kwa hivyo, baada ya kuzingatia hali ya kesi hii, ombi hili limewasilishwa kimakosa na ni jaribio la kuipatia mahakama hii mamlaka ambayo haina. Njia pekee baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa ni kuendelea na kesi iliyo mbele ya mahakama hii,” alisema Jaji Nduma.
Mahakama ilisema ni kwa maslahi ya haki na usawa kwamba kesi hiyo, ambayo iliwasilishwa mwaka 2023, iendelee kusikilizwa.
Meta walidai kuwa rufaa yao katika Mahakama ya Juu ina masuala ya tafsiri ya Katiba, hivyo ilikuwa muhimu kesi hiyo isitishwe hadi Mahakama ya Juu itakapotoa mwelekeo.
Kampuni hiyo kubwa ya mitandao ya kijamii ilipinga kuwa wasimamizi wa maudhui wa Facebook hawawezi kuwashtaki kwa kuwa Meta haina ofisi wala shughuli zozote nchini Kenya, hivyo si waajiri wao. Meta walionya kuwa wanaweza kulazimika kulipa Sh10 milioni kwa wafanyakazi ambao si wafanyakazi wao rasmi.
Walisisitiza kuwa Katiba ya Kenya haiwezi kutumika nje ya mipaka ya kijiografia ya taifa hilo na hivyo mahakama haina mamlaka ya kushughulikia kampuni ya kigeni kama Meta.
Hata hivyo, mnamo Machi 20, 2023, Jaji Nduma aliruhusu wafanyakazi hao kukabidhi Meta stakabadhi za kesi katika makao yao makuu nchini Amerika. Baada ya Meta kukata rufaa, Mahakama ya Rufaa pia ilitupilia mbali kesi hiyo na kusema kuwa vitisho vya kufutwa kazi kwa wasimamizi hao vinashughulikiwa na ELRC.
Wasimamizi wa maudhui hao, kupitia wakili wao Mercy Mutemi, walieleza kuwa Meta na ajenti wake wa zamani Samasource Kenya EPZ walizindua mpango wa kuwafuta kazi kwa kulipiza kisasi baada ya Daniel Motaung kutoka Afrika Kusini kuwasilisha kesi akilaumu kampuni hiyo kwa mazingira duni ya kazi.
Bi Mutemi alisisitiza kuwa Meta na maajenti wake wanafanya biashara nchini Kenya, kwamba Facebook ina mamilioni ya watumiaji nchini humo, na hupata mapato kupitia huduma kama Facebook Pay na Facebook Marketplace.