Jaji azima EACC kumkamata Wamatangi kwa madai ya ufisadi
GAVANA wa Kiambu Kimani Wamatangi amepata agizo la mahakama kuzuia kukamatwa siku chache tu baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuruhusiwa kuzima akaunti za benki za kampuni tano zinazodaiwa kuwa na uhusiano naye, kufuatia tuhuma za ufisadi.
Jaji wa Mahakama Kuu, Chacha Mwita, alitoa agizo la muda kuzuia Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga, na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), kumkamata au kumfikisha mahakamani Bw Wamatangi kutokana na madai ya ufisadi.
“Agizo linatolewa kuzuia washtakiwa kukamata na kushtaki mlalamishi kwa msingi wa uchunguzi uliofanywa katika kesi hii hadi Septemba 18, 2025,” jaji alisema.
Hata hivyo, Jaji Mwita alikataa kuzuia uchunguzi unaoendelea unaofanywa na EACC akisema tume inatekeleza mamlaka yake.
Wiki iliyopita, Jaji Lucy Njuguna alikubali ombi la EACC la kuzima akaunti tano za benki zinazohusiana na King Group Company Ltd, King Realtors Ltd, King Construction Company Ltd, Quick Fix Auto Garage Ltd, na Lub Plus Oil and Energy Company Ltd, ambazo zinadaiwa kuwa na uhusiano na Bw Wamatangi.
Tume ya kupambana na ufisadi ilisema kampuni hizo zilipewa zabuni za thamani ya Sh700 milioni wakati Bw Wamatangi alikuwa seneta wa Kiambu na mwanachama wa kamati ya Bunge la Seneti ya Barabara kati ya mwaka 2017 na 2022.
“Kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kuhifadhi fedha hizo na kuzima akaunti hizo kwa kipindi cha miezi sita hadi uchunguzi utakapokamilika na hatua za kurejesha fedha kuanzishwa,” Jaji Lucy Njuguna alisema.