Habari

Jalang’o aomba radhi kwa matamshi yake ya ‘uchawi’ Kisii

Na WYCLIFFE NYABERI April 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MBUNGE wa Lang’ata Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o amejipata pabaya kufuatia matamshi yake siku ya Jumapili katika Kaunti ya Kisii.

Mbunge huyo wa mara ya kwanza, miongoni mwa viongozi wengine, alikuwa ameandamana na Naibu Rais Kithure Kindiki kuchangisha fedha za ujenzi wa Kanisa Katoliki la Marani.

Wakati wa harambbe hiyo, Bw Jalang’o alidai kuwa alikuwa amesafiri hadi Kisii siku moja iliyotangulia na kukaa kwa muda katika eneo moja lililoko sehemu hizo.

Mcheshi huyo wa zamani alidai kwamba katika kipindi kifupi alichokaa katika mkahawa mmoja wa eneo hilo, aliona kikundi cha wanaume aliowataja kama “Baraza la Wachawi” wakizungumza kuhusu maendeleo ambayo Mbunge wa eneo hilo Japheth Nyakundi alikuwa amefanya.

Kulingana na Bw Jalang’o, wanaume hao ambao alisema walikuwa 12 hivi, walikuwa na uchungu kwamba mbunge huyo alikuwa ameunganisha wakazi wake wengi na umeme, hivyo basi kufanya tabia yao ya “kutembea” usiku kuwa ngumu kwani wangeweza kuonekana kwa urahisi kwenye mwangaza.

“Nilifika hapa mapema, nililala hapa Marani, sehemu iitwayo Marani Simba Lodge. Nikiwa huko niliona kundi la wanaume wakiwa na baraza, watu wapatao 12 walikuwa wakizungumza, nikasema ngoja nisikilize hawa watu ni akina nani, nikagundua kuwa ni baraza la wachawi, walikuwa wachawi ambao walikuwa wakijadiliana kuwa Bw Nyakundi ameunganisha kila kona ya eneo lake na umeme uliokuwa ukiwamulika,” Bw Jalang’o alidai.

Punde tu baada ya kutoa semi hizo, Wakenya walimiminika kwenye mitandao ya kijamii kumshutumu, wakisema kuwa matamshi yake yalikuwa ya kuudhi sana na yale yakisawiri jamii katika hali mbaya. Walimtaka kuomba msamaha watu wa Gusii kwa matamshi yake ya Jumapili.

“Leo, Phelix Odiwuor a.k.a Jalang’o Mwenyewe aliwadharau watu wa Marani. Nikiwa mwana wa Marani mwenye kujivunia, naona maneno yake yanachukiza sana. Tangu nizaliwe, sijawahi kuona mambo kama haya kwa macho yangu. Inakuwaje mgeni anadai kuwa ameyaona? Sisi Wakisii ni watu wachapakazi sana, sio vile anavyosema Jalang’o,” mwanamuziki maarufu wa Gusii Man Sango alisema.

Kuna wale ambao hata hivyo wamejitokeza kumtetea mbunge huyo, wakisema kuwa hakuwahi kudhalilisha jamii ya Gusii kwa dhana kama hiyo.

“Jalang’o Mwenyewe alikuwa anajaribu tu kuwa mcheshi jinsi alivyo, sisi tuliokuwa uwanjani tuliona ucheshi wake,”  Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Bidhaa Duke Mainga Echate alisema.

Bw Jalang’o amejibu shutuma hizo, akisema kuwa maoni yake yalipotoshwa na kwamba hatawahi kushambulia mtu yeyote.

“Nimeona ripoti kuhusu kile kilichosemwa wakati wa ziara yangu ya Kisii, na nimeumizwa sana na jinsi maneno yangu yalivyopotoshwa. Inaniuma kusikia kwamba kuna mtu yeyote angefikiria ningetusi au kudharau jamii ya Kisii. Hivyo sivyo nilivyo,” mbunge huyo alisema.

Mbunge Jalang’o ni kiongozi wa hivi punde kuwahi kutoa matamshi yanayoonekana kuibua hisia miongoni mwa watu kuhusu masuala tata.

Mapema mwezi huu, Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Junior alilazimika kuomba msamaha baada ya matamshi yake kuhusu Kaunti ya Homa Bay kuhusu maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Akiwaaga vijana wa Makueni, waliopaswa kuhudhuria Michezo ya Kenya Youth Inter-County Sports Association (KYISA) katika Kaunti ya Homa Bay, gavana huyo alitoa ujumbe wa tahadhari akiwataka vijana hao kuwa waangalifu wakiwa katika gatuzi hilo.

Katika tahadhari yake, Bw Mutula alirejelea takwimu za kaunti hiyo kuhusu zimwi la Ukimwi.

Matamshi ya Gavana Mutula yalizua hisia tofauti, huku wengine wakimtuhumu kwa kuinyanyapaa kaunti hiyo na wakazi wake bila kukusudia.

Ilimbidi gavana huyo kuomba radhi.