JAMII moja katika eneo la Rangwe, Kaunti ya Homa Bay, imeshikilia msemo kwamba kutoa ni moyo na usambe ni utajiri na vile vile umoja ni nguvu utengano ni udhaifu, katika jitihada zao za kuhakikisha kila mwana wa hapo anapokea masomo.
Katika kijiji cha Kowili, Wadi ya Kochia, ikiwa ni elimu kila mtu lazima ahakikishe kuwa watu wao na wale wa majira wanaenda shuleni.
Kama watu wa ukoo mmoja, walibuni njia bunifu ya ambapo kila mtu huchanga pesa alizonazo kwa ajili ya kupelekwa katika shule kugharamia karo ya watoto kutoka familia masikini.
Usaidizi huo utatolewa chini ya mwavuli wa wakfu wa Kowili Education Recovery Foundation katika Kata ya Kochia Central.
Mwenyekiti wa wakfu huo Kennedy Ogindo anasema kuwa lengo la ni kuhakikisha kuwa watoto kutoka koo zote katika kata hiyo wanapata masomo.
“Wale walioacha shule katika kiwango cha shule ya msingi na vyuo vya kadri wanasaidiwa kurejea masomoni kuendeleza ndoto yao,” anasema.
Kundi hilo lilibuniwa na kuanza mipango yake mnamo 2022. Hii ni pale wakazi walipogundua kuwa baada ya watoto huacha masomo kutokana na changamoto kadha, hususan, ukosefu wa karo.
Bw Ogindo anasema waathiriwa wakubwa ni watoto mayatima ambao hawana wa kuwasaidia hata kupata mahitaji ya kimsingi kama chakula na mavazi.
Tangu kilipobuniwa kundi hiyo hushirikiana na viongozi wa mashinani na wale wa serikali kukusanya fedha za kulipa karo ya watoto kutoka familia masikini.
Mwaka huu kikundi kilikusanya jumla ya Sh3.3 milioni.
“Mwaka jana, tulikusanya Sh3 milioni na tukazitumia kulipia karo ya jumla ya watoto 566 kutoka familia masikini,” Bw Ogindo akaeleza.
“Mahitaji ya kila mwanafunzi huwa tofauti na ndio maana huwa hawapati kiasi sawa. Wengine hulipiwa karo yote ilhali baadhi yao wakilipiwa sehemu ya karo,” anaeleza.