Habari

Jaribio la al-Shabaab kuteka gari la polisi latibuka

December 20th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na KALUME KAZUNGU

MAAFISA wa usalama Jumapili wamezima shambulio la wapiganaji wa al-Shabaab waliokuwa wamevamia gari la polisi eneo la Nyongoro, karibu na Lango la Simba katika barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen.

Shambulio hilo lilitekelezwa saa tano asubuhi.

Kamanda wa Polisi, Kaunti ya Lamu, Moses Murithi amesema mojawapo ya magari ya polisi wa kikosi cha kushika doria mipakani (BPU) yaliyokuwa yakisindikiza mabasi ya usafiri wa umma kutoka Lamu kuelekea Gamba na Mombasa lilivamiwa na wapiganaji hao waliokuwa wamejihami vikali.

Makabiliano ya risasi kati ya polisi na wapiganaji yalizuka na kudumu kwa zaidi ya dakika kumi kabla ya al-Shabaab kushindwa nguvu na kutorokea kwenye msitu wa karibu.

Bw Murithi amesema hakuna aliyejeruhiwa wala kuuawa wakati wa makabiliano hayo. Alisema maafisa wa vikosi mbalimbali vya usalama, wakiwemo wale wa jeshi (KDF) na polisi tayari wametumwa kwenye eneo husika ili kuwasaka wahalifu hao.

Kamanda huyo wa polisi aidha amewahakikishia wakazi, hasa watumiaji wa barabara ya Lamu kuelekea Garsen na Mombasa kwamba usalama wao umedhibitiwa, hasa wakati huu ambapo ni msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

“Kumekuwa na shambulio la al-Shabaab kati ya Nyongoro na Lango la Simba kwenye barabara kuu ya Lamu kuelekea Garsen na Mombasa. Gari la polisi wa kikosi cha BPU lililokuwa likisindikiza mabasi ya abiria kutoka Lamu kuelekea Gamba na Mombasa limevamiwa na wapiganaji hao,” akasema Bw Murithi.

Shambulizi hilo linajiri wakati ambapo wasafiri kwenye barabara ya Lamu kuelekea Mombasa wamekuwa wakiisifu idara ya usalama eneo hilo kwa kukabiliana na kupunguza mashambulizi na mauaji ya kila mara yaliyokuwa yakitekelezwa na Al-Shabaab barabarani.

Mbali na uvamizi wa Jumapili, shambulizi la mwisho kuwahi kutokea kwenye barabara hiyo ya Lamu ni lile la Januari 2 mwaka huu, ambapo watu watatu waliuawa ilhali wengine watatu wakijeruhiwa pale magaidi wa Al-Shabaab walipovamia mabasi ya usafiri wa umma yaliyokuwa yametoka Mombasa kuelekea Lamu na kuyamiminia risasi eneo hilo hilo la Nyongoro.