Habari

Jinsi msamaha wa ushuru wa ‘kufurahisha wapiga kura’ umeweka kaunti pabaya

Na ERIC MATARA March 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HUKU serikali za kaunti zikitazika kufikia malengo ya mapato, msamaha wa ‘kisiasa’ unaohusu ukusanyaji wa ushuru inazinyima mamilioni ya pesa, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imefichua.

Baadhi ya magavana wamekuwa wakifutilia madeni ili kuwafurahisha wapiga kura na kunyima kaunti zao mapato inayohitaji, na kuacha kaunti zikitegemea sana mgao kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bi Nancy Gathungu kwa mwaka wa kifedha wa 2022/2023 na 2023/2024, inafichua kutojitolea kwa baadhi ya kaunti katika ukusanyaji wa mapato na kusababisha hasara kubwa.

Miaka 13 tangu ujio wa ugatuzi, serikali za kaunti zinaendelea kupoteza mabilioni ya pesa kutokana na wizi na mifumo mibovu na isiyoeleweka ya kukusanya mapato.

Zaidi ya robo tatu ya kaunti 47 za Kenya bado zinatatizika kufikia malengo yao ya mapato na kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya Tume ya Ugavi wa Mapato, kaunti zina uwezo wa kukusanya Sh260 bilioni kila mwaka lakini sasa zinakusanya chini ya Sh80 bilioni.

Mkaguzi amenyoshea Kaunti ya Kisii, kidole cha lawama kwa kutojitolea katika ukusanyaji wa mapato.

Ukaguzi wa rekodi za mwaka wa kifedha wa 2023/2024 ulifichua kuwa kaunti ilipanga kukusanya jumla ya Sh25 milioni kutoka kwa ada za ardhi katika mwaka ulioangaziwa, lakini ilikusanya Sh18milioni pekee, na kusababisha upungufu wa Sh 6.8milioni.

Kaunti ya Nakuru imekuwa ikitatizika kukusanya mapato na iliweza kukusanya kati ya Sh3 bilioni na Sh3.6 bilioni.

Kwa mfano, wakati Gavana Kihika alipoingia madarakani mwaka wa 2022, ukusanyaji wa mapato ya kila mwaka ulifikia Sh3.2bilioni.

Katika mwaka wa fedha uliopita, Bi Kihika alifanikiwa kuongeza mapato hadi Sh3.6 bilioni.

Hivi majuzi, mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Uhasibu wa Umma Moses Kajwang alifichua kuwa Kaunti ya Nakuru ambayo ina jiji, haiwezi kujiendeleza kwa kuwa inatumia Sh6 bilioni kwa mishahara na marupurupu mengine.

Hii inamaanisha kuwa kaunti kupitia mapato yake yenyewe haiwezi kumudu hata malipo ya mishahara kwa wafanyikazi pekee.

Kaunti zingine zilizoathiriwa ni pamoja na Baringo, Kilifi, Nairobi, Kisumu na Kiambu, ambazo zinadai mamilioni ya ushuru wa ardhi, lakini juhudi ndogo zimefanywa kupata malimbikizo hayo.

Kaunti zimelazimika kutoa msamaha na kupoteza mapato.