Habari

Jinsi serikali inavyolenga kuwaongoza Wakenya kutupilia mbali mitumba

July 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

MIAKA ya tisini (1990s), mashirika ya kifedha ya Ulimwengu (Bretton Woods Institutions) yaliwekea mataifa ya Afrika Masharti ya kuweka huru sekta ya nguo na matokeo yakawa mataifa ya Magharibi kujaza masoko ya Afrika na nguo kuukuu maarufu mitumba.

Sekta za utengenezaji nguo mpya Afrika zilisambaratika kwa kasi kwa kuwa mtumba uliingia ukiwa wa bei nafuu na kujishindia umaarufu katika udhaifu wa pato wa Waafrika wengi.

Masharti hayo yakifahamika kama Structural Adjustment Programmes (SAPs) yaliathiri vibaya taifa la Kenya miongoni mwa mengine, ambapo sekta ya pamba ilisambaratika kwa kuwa Wakenya walisusia nguo mpya na kuingia kwa uteja wa mitumba.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa sekta hii ya nguo mpya pamoja na ile ya pamba zilirekodi kusambaratika kwa asilimia 80.

Sasa, serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetenga Sh1.5 bilioni za kufufua sekta hii na ambapo kipau mbele kinapewa ukuzaji pamba ili kuweka sekta ya manguo mapya katika mkondo wa ufufuzi.

“Hatuwezi tukaongea kuhusu kufufua viwanda vya kushona nguo mpya bila kwanza kuzingatia malighafi ya kuvifufua. Tena, tukianza na ukuzaji pamba, tunahakikishia uchumi wetu manufaa halisi kwa kuwa tutawapa wakulima pato na viwanda vipate malighafi kutoka papa hapa nchini badala ya kuagiza kutoka mataifa jirani,” anasema Waziri wa Kilimo, Mwangi Kiunjuri.

Aliambia Taifa Leo kuwa kwa sasa Wakenya wanazalisha beli 20,000 za pamba kwa mwaka, hali ambayo anaitaja kuwa duni zaidi.

Alisema kuwa hali hii ya kupunguka kwa uzalishaji ni athari za masharti yale ya 1990s na ambayo kwa sasa serikali imeazimia kuyashughulikia kwa kina.

Tanzania kwa sasa huzalisha beli 700,000 za pamba, Uganda ikizalisha beli 200,000 na hivyo basi kuwa na soko nchini Kenya hasa katika sekta ya utengenezaji wa chakula cha mifugo ambapo mbegu za mmea wa pamba hutumika kama malighafi.

Kwa mujibu wa Bw Kiunjuri, sekta ya kilimo cha pamba itagaiwa Sh300 milioni ili kuipa ushawishi wa kupandhisha mavuno hadi beli 300,000 kwa mwaka.

Hali hii, alisema kuwa itawafaa wakulima 1.3 milioni katika Kaunti 22 za hapa nchini, Sh700 milioni zielekezwe katika ufadhili wa viwanda vya pamba masalio yakielekezwa katika kupiga jeki viwanda vidogovidogo vya makundi ya vijana kujipenyeza katika riziki katika sekta hii.

Bw Kiunjuri alisema kwa sasa ufufuzi wa kiwanda cha Rift Valley Textiles (Rivatex) umeweka soko wazi la pamba la beli 100,000 na ambapo katika kipindi cha chini ya miezi sita, soko hilo litapanuka kuwa la beli 200,000 na kutoa kazi za moja kwa moja kwa watu 3,000 na ujumla wa watu 300,000 katika ujumlishaji wa manufaa halisi ya sekta yote ya pamba na viwanda vya kuitumia kama malighafi.

Kabla ya mwaka 2020 kuingia, Kiunjuri anasema kilo moja ya pamba itakuwa ikinunuliwa kwa bei ya Sh100 ikilinganishwa na hali ya sasa ya kati ya Sh45 na Sh60.

Halmashauri ya ustawishaji sekta ya pamba nchini (KCDB) tayari imesema imekadiria kuwa pamba inaweza kuwa na soko kubwa hapa nchini katika sekta zingine ambazo huitegemea kama malighafi.

Kwa mfano, zao la pamba hutumika katika sekta ya utengenezaji nguo, hutumika pia katika kiwanda cha kutengeneza risasi kilichoko Mjini Eldoret na pia katika utengenezaji wa chakula cha mifugo.

Imesema kuwa kilimo cha pamba kinaweza kikapanuliwa hadi kukumbatiwa na kaunti karibu zote nchini.

Katika harakati hizo, hekari 400,000 za ardhi chini ya kilimo hicho zitaimarishwa huku serikali ikijizatiti kuondoa mawakala ambao husambaratisha bei kwa wakulima.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bw Anthony Mureithi alisema kuwa mchango wa sekta ya pamba katika kuafikia malengo ya ruwaza ya 2030 ni wa kiwango cha juu.

“Tuko na uwezo wa kusaka Sh50 bilioni kama mapato kwa wakulima kwa mwaka. Inahitaji tu juhudi kamilifu zikiwahusisha wadau wa sekta,” akasema.

Aidha, alisema kuwa halmashauri hiyo inapendekeza kuongezwa kwa ushuru unaotozwa bidhaa za mutumba ili kutoa nafasi ya viwanda vya hapa nchini kufufuliwa.

“Kwa sasa, uagizaji wa nguo za mitumba hapa nchini umeangusha sekta ya nguo mpya ambazo zinafaa kutengenezwa na Wakenya. Nyongeza ya ushuru itazua ushindani sawa sokoni kati ya nguo kuukuu na mitumba,” akasema.