Habari

Jirongo alivyotumia pesa kutia mafuta siasa za Kenya

Na  JOHN KAMAU, BENSON MATHEKA December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

CYRUS Jirongo aliingia katika siasa za Kenya kama upepo mkali uliokuwa vigumu kupuuzwa, na hatari kuaminiwa kikamilifu.

Kwa muda, hakuwa mtu tu bali mfumo mzima: sura changa kisiasa, na kapu la fedha wakati ambapo pesa zilizungumza kwa sauti kuliko alama za vyama.

Jirongo alipokuwa kileleni, hakupita tu kwenye siasa za Kenya; alizitia mafuta kwa pesa. Katika msimu wa uchaguzi wa vyama vingi wa 1992, akiwa mwenyekiti wa Youth for KANU ’92 (YK’92), aligeuka kuwa mashine ya fedha ya chama tawala kilichokuwa kikihangaika kuendelea kuwa madarakani.

“Kila mwanasiasa ana bei yake,” alinukuliwa akisema—kauli iliyotua kama tishio lililojificha ndani ya busara. Kwa wafuasi wake, ilikuwa uhalisia wa siasa; kwa wakosoaji, ilikuwa kukiri wazi jinsi YK’92 ilivyokusudia kununua mamlaka kama kabeji sokoni.

Kuanzia ofisi za YK’92 katika KICC hadi Anniversary Towers, fedha hazikutiririka tu—zilifurika. Zilionekana katika mikutano ya kisiasa, bahasha na mabegi kama “gharama za kurahisisha mambo”. Nchi ilishuhudia utajiri wa ghafla ambao haukuakisi hali ya uchumi nje ya msafara wa kampeni. YK’92 ilitembea kwa jeuri na kelele kiasi kwamba Wakenya waliipa noti mpya ya Sh500 jina la “Jirongo”—heshima ya ajabu na kali kwa mtu aliyekuwa kiini cha sakata hilo.

Alipofariki katika ajali ya barabarani usiku wa Ijumaa,Desemba 12 2025, Jirongo alikuwa akipambana na kesi nyingi zilizohusishwa na usimamizi wa fedha alizokusanya kupitia YK’92.
Ingawa alipanda ngazi hadi kuwa Waziri katika utawala wa Moi, sura yake ilibaki ya broka wa mamlaka—mtu wa kutaka mambo ya haraka, aliyeandamwa daima na kivuli cha YK’92.

Nguvu zake zilikuwa kubwa kiasi cha kuonekana akitembea kwa saa kadhaa na Rais Moi katika viwanja vya Ikulu tofauti nchini. Marafiki wanasema aliwahi hata kuhudhuria kikao cha Baraza la Usalama wa Taifa, ambacho huhudhuriwa na wachache sana. Inadaiwa pia kuwa akiwa YK’92, alikuwa akitembea na mabomu ya mkono ndani ya gari lake.

Ikiwa ufisadi wa miaka ya 1990 ungevaa uso wa ujana, basi ungekuwa wa Jirongo—aliyetumia ukuruba wake kushawishi vijana kudhoofisha upinzani kwa wanasiasa kuhama vyama, vitisho na, kwa madai ya wengine, vurugu.
Kuandika kuhusu Jirongo ni kurejea kipindi tata cha mpito wa Kenya kuelekea demokrasia ya vyama vingi, wakati ambapo maadili yalikuwa  tu katika hotuba, lakini upendeleo ulitawala.

Swali linalosalia hadi leo ni moja: fedha za YK’92 zilitoka wapi?
Hakuna anayejali kwamba YK’92 ilitumia fedha nyingi kupita kiasi. Haikufadhili kampeni pekee, bali iligeuza siasa kuwa tamasha. Wapiga kura walisafirishwa kwa malori na mabasi, wakaburudishwa na mara nyingine kulipwa pesa taslimu. Mabango, fulana na kofia zilifurika masokoni.

Katika kilele cha shamrashamra hizo, Goldenberg International—kampuni ya Kamlesh Pattni na James Kanyotu—iliendelea kufaidika kutoka Benki Kuu ya Kenya kwa madai ya “fidia” ya dhahabu feki.

Hazina ya  NSSF iligeuzwa kuwa chanzo cha fedha za kisiasa, ikinunua ardhi iliyoporwa kwa bei ya juu kupita kiasi. Mashirika ya umma yaligeuzwa mashine za kampeni.

Jirongo, kupitia kampuni yake ya Sololo Outlets, alitajwa kupata zabuni ya kujenga nyumba za NSSF. Kamlesh Pattni aliambia tume iliyochunguza Goldenberg kuwa alifadhili YK’92, lakini  kwamba serikali yenyewe ilifungua milango ya fedha bado inaendelea kuandama historia.

Bunge ilielezwa kuwa NSSF ilinunua mali mbili za Sololo kwa Sh1.2 bilioni, zaidi ya thamani yake halisi.

Zaidi ya Sh2.5 bilioni zilidaiwa kupitishwa kupitia Post Bank Credit, benki iliyokuwa tayari taabani, hatua iliyochangia kuporomoka kwake.

Takwimu hizi zilionyesha ukweli mmoja: fedha za YK’92 hazikutokana na utajiri wa kawaida. Katikati ya yote alikuwa Cyrus Jirongo—kama mnufaika mkuu, mpangaji na mhandisi mkuu wa mpango huo.

Baada ya uchaguzi wa 1992, YK’92 ilianza kuwatisha wale waliokuwa wamenufaika nayo.

Ilionekana kama kituo cha mamlaka kisichodhibitika. Hatimaye, Rais Moi alisitisha shughuli zake mwaka 1993 baada ya Jirongo kumshambulia hadharani Makamu wa Rais George Saitoti.

Kisha mfumo ukaonyesha upande wake mwingine wa kuadhibu. Kampuni zake ziliwekwa chini ya usimamizi maalum, zikapokonywa zabuni, na madai ya ushuru yakafuata. Hata hivyo, ni wachache waliokabiliwa na mashtaka ya jinai.

Licha ya yote, Jirongo hakutoweka.

Alihudumu kama Mbunge wa Lugari mara mbili na akaendelea kuwa katika ulingo wa siasa. Lakini jina lake lilibaki kuibua kumbukumbu za pesa nyingi, kesi nyingi na maswali yasiyojibiwa.

Kwa msingi huu, Cyrus Jirongo anabaki kuwa alama zaidi ya mtu: broka wa mali aliyegeuka wa kuamua wafalme, kijana aliyegeuka radi ya kisiasa. Kukwea kwake ngazi ya ushawishi  kunaonyesha nguvu ya upendeleo; kuporomoka kwake kunaonyesha ukatili wa mfumo huo huo. Na ikiwa Kenya itataka kufunga ukurasa wa “Jirongo” kama jina la noti ya pesa, haitakuwa kwa kumsahau mtu huyo—bali kwa kurekebisha mfumo uliomruhusu kuwepo.