Habari

JKIA yafungwa kwa muda baada ya waombolezaji kuvuruga usalama

Na CHARLES WASONGA October 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SHUGHULI katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) zimesitishwa kwa muda baada ya waombolezaji kuvuruga usalama humo mwili wa Hayati Raila Odinga ulipokuwa ukiwasili.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Alhamisi, Oktoba 16, 2025, Mamlaka ya Kusimamia Safari za Angani (KCAA) ilisema ililazimika kuchukua hatua hiyo baada ya waombolezaji kuingia sehemu zisizoruhusiwa katika uwanja huo.

“KCAA inajulisha umma kwamba shughuli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta zimesitishwa kwa muda kutokana na hali ya usalama iliyoshuhudiwa kufuatia kufika kwa mwili wa Mheshimiwa Raila Odinga,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa KACC Emile Arao.

Mamlaka hiyo ilitoa wito kwa umma na wasafiri kusalia watulivu na kutofika katika uwanja huo wa ndege hadi mwelekeo utakapotolewa baadaye.

“Shughuli za kawaida zitarejelewa baada ya uwanja wa JKIA kutangazwa kuwa salama,” Bw Arao akasema.

Ndege ya Shirika la Ndege Nchi (KQ)  iliyobeba mwili wa Raila ilipowasili katika uwanja huo, maelfu ya waombolezaji walionekana kuwalemea maafisa wa vikosi mbalimbali vya usalama.

Isitoshe, baadhi yao, waliokuwa wakilia kwa sauti wakibeba matawi, walionekana karibu zaidi na ndege hiyo iliyopewa jina “RAO OO1”.

Ilikuwa ni vigumu kwa Rais William Ruto, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na viongozi wengine kuupokea rasmi mwili wa mwendazake.

Kando na hayo, shughuli za kijeshi zilizoratibiwa kufanyika katika uwanja wa JKIA wakati kupokewa kwa mwili huo pia zilifutiliwa mbali.