Habari

Joho agawanya Waislamu

January 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MOHAMED AHMED

VIONGOZI wa dini ya Kiislamu wamewakosoa wanasiasa kwa kumtawaza Gavana Hassan Joho wa Mombasa kuwa kiongozi wa Waislamu nchini.

Wahubiri hao walipinga hatua hiyo wakisema ni kinyume na mienendo ya dini na pia hapakuwa na mashauriano ya kuamua atakayeongoza Waislamu katika masuala ya siasa.

Hii ni kufuatia hatua ya viongozi wa kisiasa kutoka eneo la Kaskazini Mashariki kumtaja Bw Joho kuwa mwenye nguvu za kuongoza Waislamu kitaifa.

Wakiongozwa na Mbunge wa Fafi, Abdikarim Osman, viongozi hao walimtawaza Bw Joho wakati wa mkutano wa BBI katika bustani ya Mama Ngina, Kaunti ya Mombasa mnamo Jumamosi.

“Bw Joho sio kiongozi wa Pwani pekee, bali anayetosha kuwa kiongozi wa Waislamu wote nchini,” akasema Mbunge wa Fafi, Abdikarim Osman alipowaongoza viongozi wenzake kumvisha Bw Joho magwanda ya uongozi.

Mwekahazina wa Baraza la Maimamu na Wahubiri Nchini (CIPK), Sheikh Hassan Ibrahim alisema hakuna jinsi mwanasiasa anaweza kutawazwa kuwa kiongozi wa dini.

“Joho ni mwanasiasa na hawezi kuwa kiongozi wa dini. Hayo maneno ni ya wanasiasa. Kama ni kisiasa, hiyo ni sawa kwa mtazamo wao wenyewe lakini sio kwa kila Mwislamu,” akasema Sheikh Ibrahim.

Alisema kuwa ili kiongozi awe anaweza kuongoza waumini lazima maafikiano yawepo miongoni mwa viongozi wa kidini.

Mwenyekiti wa Kitaifa wa Baraza la Ushauri wa Waislamu wa Kenya (Kemnac), Sheikh Juma Ngao, alisema hatua ya utawazo kama huo inahitaji mashauriano kwanza, kwani kuna wanasiasa wengine Waislamu waliohitimu kutawazwa kuwa viongozi.

“Sisi kama viongozi wa dini tutakuwa tunajivunia kuwa na kijana wa Pwani kuongoza wanasiasa wengine wa dini ya Kiislamu. Joho hawezi kuwa kiongozi wa dini bali wa kisiasa pekee,” akasema Sheikh Ngao.

Alisema viongozi wengine ambao wanatoka dini hiyo na wamekuwa kwenye ulingo wa siasa kwa muda mrefu na wangejumuishwa kabla ya uamuzi wa kumtawaza Bw Joho.

Alimtaja Seneta wa Garissa, Yusuf Hajji kama mfano wa viongozi wakongwe wa dini ya Kiislamu ambao wamekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu.

Bw Joho anatazamwa na wengi kuwa kigogo wa kisiasa Pwani anayetarajiwa kuwania uongozi wa eneo hilo endapo katiba itarekebishwa kuweka serikali za majimbo.

Katika mkutano wa Jumamosi ambao uliongozwa na kinara wa ODM Raila Odinga, viongozi wa Pwani waliwasilisha matakwa ambayo walitaja ni yale ambayo Wapwani wanataka yazingatiwe na Jopo la Maridhiano (BBI).

Akisoma mapendekezo ya wanasiasa wa Pwani kwa niaba ya viongozi hao wengine, Gavana wa Kilifi Amason Kingi alisema Pwani inafaa kutengewa majimbo mawili.

“Tunataka Pwani igawanywe ili iwe na wasimamizi wa Pwani ya Juu na ule wa Chini,” akasema Bw Kingi katika mkutano huo wa Jumamosi.

Katika mgawanyo huo, kaunti za Taita Taveta, Mombasa na Kwale zinapendekezwa kuwa katika upande wa Pwani ya Chini na kaunti za Lamu, Kilifi na Tana River ziwe katika Pwani ya Juu.

Pendekezo hilo limeonekana kuwa la Bw Kingi na Bw Joho, ambao wapo katika hatamu zao za mwisho kama magavana kujitafutia nafasi za uongozi kipindi chao kikiisha 2022.

Katika mpangilio huo, Bw Joho anatarajiwa kuwania kuwa kiongozi wa Pwani ya Chini naye Bw Kingi wa Pwani ya Chini.