Habari

Joho asimulia jinsi alivyoteseka akiwa mtoto

August 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

Na MARY WANGARI

GAVANA wa Kaunti ya Mombasa Ali Hassan Joho amewapa matumaini wengi, hii ikiwa ni baada ya yeye kusimulia safari yake tangu utotoni, kuwa mchuuzi wa vitumbua, hamali hadi kiongozi maarufu jinsi alivyo hii leo.

Katika mahojiano Jumapili, Gavana huyo alisimulia jinsi alivyolelewa na mamake ambaye kwa sasa ni marehemu, baada ya kutengana na baba yake aliyekuwa mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) na mchezaji kandanda maarufu.

“Niliishi na mama yangu maisha yangu yote baada ya wazazi wangu kutengana. Mamangu alikuwa rafiki yangu wa dhati, alinifanya kuwa jinsi nilivyo, alinifunza mambo mengi kuhusu maisha, alinielekeza, kunishauri na kunifanya mwanamume anayeelewa maisha,” akasimulia Joho.

Akaendelea: “Kwa hakika nimekuwa na marafiki wengi; nina marafiki wa dhati lakini sijawahi kuwa na rafiki wa karibu kushinda marehemu mamangu. Alikuwa kila kitu kwangu, alihangaika kwa sababu yangu. Aling’ang’ana maishani na alitulea kwa taabu sana.”

Gavana Joho alikumbuka siku moja akiwa katika shule ya msingi ambapo mama yake alikamatwa na polisi kwa kuendesha kioski bila leseni.

“Siku ambayo sitawahi kusahau maishani ni wakati niliona mamangu akikamatwa na polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi cha Makupa kwa kuendesha kioski bila leseni na singeweza kufanya chochote wakati huo, nilikuwa katika shule ya msingi. Nikikumbuka huwa inaniuma sana lakini alipitia yote hayo ili aweze kutulisha,” alieleza gavana.

Kulingana naye, mamake alikuwa muumini wa dhati ambaye hangemruhusu kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa huku akisimulia jinsi alivyomnasa wakati mmoja akiwa mbunge na akalazimika kumsihi asimwaibishe hadharani.

Gavana huyo alizuru nyumba alimozaliwa na kulelewa katika miaka ya 1970 pamoja na ndugu zake hadi walipohama baadaye akiwa katika Darasa la Saba.

“Hapa ndipo nilipozaliwa na kuishi maisha yangu yote nikiwa katika shule ya msingi. Nilipokuwa nikienda Darasa la Saba ndipo tulihama. Nyumba hii ingali mali ya familia, tumeiweka tu na tuna nia ya kuendelea kuiweka hivi ili tusisahau pale tulipotoka,” alisema.

Bosi huyo wa kaunti alikumbuka siku zake za utotoni alivyolelewa katika jamii iliyoshikilia maadili ya ujamaa na undugu, ambapo kila mmoja alimfahamu mwingine na hata kuweza kuomba chumvi kirahisi kupitia dirishani.

“Maisha enzi hizo yalikuwa tofauti kabisa. Tulikuwa na yale maadili ya ujamaa na undugu. Nakumbuka majirani zangu wote, jinsi tulivyokua, tulivyokuwa tukicheza, nani alikuwa jirani yangu katika upande huo mwingine,”

“Maadili ya kijamii enzi hizo yalikuwa tofauti kabisa na siku hizi. Tulikuwa na dirisha kwenye sehemu ya nyuma ya nyumba tulizokuwa tukitumia kuwasiliana na kupiga gumzo. Ukihitaji msaada, ukihitaji chumvi, ukihitaji mafuta, ukitumwa na mama au nyanya yako, unapitia tu dirisha moja hadi nyingine,” alieleza.

Mwanasiasa huyo alikuwa na kumbukumbu za dhati kuhusu marehemu nyanya yake aliyekuwa akiandaa vitumbua kila adhuhuri ambapo Bw Joho akiwa mtoto alikuwa akitwikwa jukumu la kupakia, kubeba na kuuza, alifichua hapo ndipo alitia makali ujuzi wake wa kibiashara.

“Hapo pembeni ndipo nyanyangu marehemu alikuwa akiandaa vitumbua kila adhuhuri. Angevitayarisha usiku ambapo mwendo wa saa tisa, saa kumi alikuwa tayari ameshamaliza. Kila niliporejea kutoka shuleni, kazi yangu sasa ilikuwa kupakia, kubeba na kuanza kuchuuza.

“Hata mkileta stori za kuuza vitu mimi naweza kuwashinda mbaya sana nikianza hapo nilikuwa naanza tu vitumbua, vitumbua, vitumbua,” alisimulia gavana huyo anayefahamika miongoni mwa wafuasi wake kama 001.

Aidha, alikumbuka kuhusu ukarimu wa marehemu mjomba wake aliyewawekea mfereji wa kuogea, choo cha kukalia na kisha kuezeka nyumba yao kwa mabati jambo waliloonea fahali si haba wakiwa watoto.

Alisimulia jinsi kaka kalivyofanya kazi kama hamali akiwa katika Kidato cha Tatu ambapo angepakia na kupakua mizigo katika Ufuo wa Utange,, kazi aliyoonyeshwa na kaka yake.

“Kakangu mkubwa alinishika mkono. Anajua, yeye ni zaidi ya kaka. Watu husema mambo mengi kuhusu kakangu. Lakini alijitwika nafasi ya baba. Tunamheshimu na kumpenda kwa mchango wake katika maisha yetu. Ni yule mtu anajitolea alikuwa akipata Sh2,000 na kutupatia familia yake Sh1,950 au wakati mwingine zote,” alieleza.