Habari

Joho sasa amtaka Ruto amalize ‘kumi bila breki’

Na KALUME KAZUNGU March 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAZIRI wa Madini, Uchumi wa Baharini na Masuala ya Ubaharia, Bw Hassan Joho, ametangaza msimamo kwamba ataunga mkono Rais William Ruto kwa urais ifikapo mwaka wa 2027.

Kauli hii ya Bw Joho imejiri wakati ambapo baadhi ya viongozi na wanachama wa ODM Pwani wanataka kinara wao, Bw Raila Odinga, ajitose tena kwenye debe katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akiongea alipokuwa ziarani Lamu, Bw Joho, ambaye ni mmoja wa wandani wakuu wa Bw Odinga, alisema hafurahi kuwaona wanasiasa wakipinga serikali licha ya Rais Ruto kujikaza na kutekelezea Wakenya maendeleo, hatua ambayo utawala wa awali ulishindwa kufanya.

“Mko na serikali, chini ya Rais William Ruto, ambayo inatoa huduma kwa wote kwa kuzingatia usawa wa kimaeneo. Ndiyo sababu nitazidi kumuunga mkono Rais Ruto kuona kwamba anapata hatamu ya pili ifikapo 2027,” akasema Bw Joho.

Hata hivyo, alifafanua kwamba azma yake ya kuongoza taifa siku za usoni pia bado ipo.

Alikuwa akizungumza wakati alipoongoza uzinduzi wa mradi wa Sh255 milioni wa maegesho ya wavuvi kwenye jeti ya Mokowe mnamo Jumatano.

Bw Joho, Naibu Gavana wa Lamu, Mbarak Bahjaj na Katibu wa Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Bahari, Bi Betsy Njagi wakati wa uzinduzi wa mradi wa maegesho ya wavuvi wa Mokowe, Lamu, Jumatano Machi 5, 2025. Mradi huo utagharimu Sh255 milioni. Picha|Kalume Kazungu

Kwenye hotuba yake, Bw Joho alisisitiza kuwa, endapo mtu ni kiongozi na anapofaulu kutekeleza maendeleo kwa kuzingatia usawa wa kimaeneo, mjadala unaosalia mara nyingi huwa ni ule wa usawa wa kisiasa.

Alisema serikali imeonyesha nia ya kutekeleza miradi ya maendeleo katika kila pembe ya nchi bila kujali waliounga mkono Kenya Kwanza wala upinzani katika uchaguzi uliopita.

“Umeme ukiwashwa Kakamega pia utapata serikali ikiuzindua Ndau (Lamu). Tuache hizi siasa za ukabila na dini na tuwe kitu kimoja kuleta maendeleo nchini. Wakati wa siasa ukifika mjue tutapiga siasa. Msisahau kuwa hata mimi Joho pia lazima siku moja niwe rais wa nchi hii,” akasema Bw Joho.

Wanasiasa wa Lamu wakiongozwa na Naibu Gavana, Dkt Mbarak Bahjaj, na Spika wa Bunge la Kaunti hiyo, Bw Azhar Mbarak, pia walikariri wito wa wananchi kumuunga mkono Rais Ruto ifikapo uchaguzi wa 2027 ili akamilishe hatamu yake ya pili.

Dkt Bahjaj alimtaja Rais Ruto kuwa kiongozi mkakamavu.

“Tuendelee kumuunga mkono Rais Ruto kutwaa uongozi ifikapo 2027. Ila tunajua wakati utafika ambapo Waziri wetu, Hassan Joho na Gavana wetu, Issa Timamy, ambao nyinyi ndio simba mngurumao Pwani, mtashirikiana na wengine na kusimamisha mmoja wenu atakayepeperusha bendera ya kitaifa siku za usoni,” akasema Dkt Bahjaj.