Habari

Jopo la Shakahola lalia hawajalipwa pesa mwaka moja baada ya kumpa Ruto ripoti

Na DAVID MWERE May 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANACHAMA wa jopo lililoundwa na Rais William Ruto kutoa mapendekezo ya kufanyia asasi za kidini mageuzi nchini sasa wanalia kuwa hawajalipwa mwaka moja baada ya kuwasilisha ripoti yao ikuluni.

Jopo hilo lilikuwa likiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Mbeere Kaskazini Kasisi Mutava Musyimi.

Lilibuniwa kupitia notisi ya gazeti mnamo Mei 5, 2023 kufuatia kufichuliwa kwa makabari ya halaiki kwenye msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi.

Makaburi hayo ya halaiki yalikuwa na miili ya waumini wa mhubiri tata Paul Mackenzie, wa kanisa la Good News International ambalo lilitoa mafunzo ya itikadi kali kwa waumini wake.

Kasisi Musyimi na wanawachama 15 wa jopo lake waliwasilisha ripoti yao kwa Rais Ruto mnamo Julai 30, 2024 kwenye ikulu ya Nairobi ambapo walipendekeza makundi ya kidini yadhibitiwe kuzuia kuenezwa kwa mafunzo ya itikadi kali.

“Tulifanya kazi yetu na kumpa Rais ripoti yetu mchana kutwa ili hatua zichukuliwe. Japo ripoti hiyo haijatekelezwa pia hawajatulipa,” akasema mwanachama wa jopo ambaye hakutaka jina lake litajwe akihofia ghadhabu za serikali.

Kando na Kasisi Musyimi, wanachama wengine wa jopo hilo walikuwa ni Askofu Mark Kariuki, Askofu Eli Rop, Askofu mkuu Maurice Muhatia, Judy Thongori (sasa marehemu), Kasisi Dkt Alphonce Kanga na Askofu Philip Kitoto.

Wengine walikuwa Dkt Faridun Abdalla, Profesa Musili Wambua, Joseph Khalende Mary Kitegi, wakili Charles Kanjama, Leah Kasera, Nancy Murega na Wilson Wanyanga. Martin Talian na Maria Nyariki walikuwa makatibu wenza wa jopo hilo.

Kasisi Musyimi hakuzungumzia kutolipwa kwao lakini akasema ni matumaini yake kuwa yaliyomo kwenye ripoti hiyo yatatekelezwa.

“Kama mzee katika jamii, maombi yangu ni kuwa mapendekezo yetu yatatekelezwa na serikali. Hatutaki kuona yale yaliyotokea Shakahola yakifanyika maeneo mengine ya nchi,” akasema Kasisi Musyimi.

Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei hakujibu jumbe zilizotumwa kwenye simu yake kutoa ufafanuzi kwa nini wanachama wa jopo hilo hawajalipwa pesa zao.

Mishahara ya majopo yanayoundwa na serikali kutekeleza wajibu mbalimbali hulipwa kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na Tume ya Kutathmini Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC).