Habari

Jubilee imekufa – Kuria

June 29th, 2019 2 min read

Na NDUNGU GACHANE

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria, ameongoza baadhi ya viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya Jubilee kutoka Mlima Kenya, kudai kwamba chama hicho kimesambaratika na hakiwezi kufufuliwa.

Bw Kuria aliwaomba viongozi wa chama hicho kuiga mfano wake kwa kuondoka kwa sababu kimezama.

“Ikiwa viongozi wanaolalamika hawaridhiki, basi waondoke kama nilivyofanya,” alisema Kuria.

Mbunge huyo anahusishwa na chama kipya cha Transformational National Alliance Party (TNAP).

Wabunge ambao walizungumza na ‘Taifa Leo’ walisema chama hicho kimeisha na ndiyo sababu mustakabali wake unayumba.

Viongozi wengine waliounga maoni ya Kuria ni Peter Kimari (Mathioya), Nduati Ngugi (Gatanga) na Bw Charles Mwangi ambaye ndiye mwakilishi wa ukanda wa Mlima Kenya katika Baraza la Mabunge ya Kaunti (CAF) na mwenyekiti wa Baraza la Chama cha Jubilee katika Kaunti ya Murang’a.

Walisema kuwa hawaoni dalili zozote za kufufuliwa kwa chama hicho na kwamba, ili kudumisha uwezo wake kisiasa kuelekea 2022, hatua ya pekee ni kubuni muungano wa kisiasa na vyama kama ODM na Wiper.

Walipozindua chama hicho, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto walisema kuwa azma yao ni kukiwezesha kudumu kwa zaidi ya miaka 20.

Kulingana na Bw Kimari, malumbano yanayokikumba yataathiri sana umaarufu wake kabla ya 2022.

“Ikiwa chama hiki hakitavunjwa na chama kipya kubuniwa, njia ya pekee kwa Jubilee ni kubuni mikataba ya kisiasa na vyama thabiti vya kisiasa kama ODM na Wiper ili kubuni serikali baada ya uchaguzi huo,” alisema mbunge huyo kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Naibu Kiranja wa Seneti Irungu Kang’ata alisema kuwa inasikitisha kuwa chama hicho kiko katika hali ya sasa, akieleza ni Bw Kenyatta na Dkt Ruto pekee wanaoweza kutuliza hali.

“Ni masikitiko kwamba tumefika tulipo kama chama. Namuomba Rais kujitokeza kutuliza joto la kisiasa lililopo. Ikiwa hawataungana, basi inamaanisha kuwa chama hiki hakipo tena,” alisema.

Kugawanyika

Bw Kang’ata alisema kuwa kuunganisha vyama vya TNA na URP ulikuwa uamuzi mzuri, akiongeza ikiwa vyama hivyo havingeunganishwa, basi nchi ingekuwa bado imegawanyika kwa misingi ya kikabila.

Bw Ngugi aliwalaumu washirika wa Dkt Ruto kwa hali ilivyo katika chama hicho, kwa kuudharau uongozi wa chama, hasa Katibu Mkuu Bw Raphael Tuju.

Licha ya juhudi za kumwomdoa uongozini ambazo zimeanzishwa na baadhi ya viongozi, Bw Tuju hajazungumzia lolote kuhusu hatua hizo.

Wakiongozwa na Seneta Samson Cherargei wa Nandi, viongozi hao wameapa kufanya kila wawezalo kumwondoa Bw Tuju mamlakani.