Habari

Juhudi za kuzima ufisadi zachacha mali ikitwaliwa

July 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

JOSEPH WANGUI Na CHARLES WASONGA

VITA dhidi ya ufisadi vinaonekana kuzaa matunda nchini baada ya Mahakama kukubaliana na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) na kutoa adhabu kali kwa wanaohusika na uovu huu.

Mwezi mmoja baada ya mahakama kuhukumu Mbunge wa Sirisia John Waluke na Grace Wakhungu, kifungo cha miaka 67 gerezani kwa kuilaghai Bodi ya Kitaifa na Mazao (NCPB) Sh340 milioni, wiki hii iliamuru kutwaliwa kwa mali ya watu wanaoshukiwa kufaidi kutokana na Sh791 milioni za shirika la NYS mnamo 2015.

Mahakama Kuu iliamuru kutwaliwa kwa nyumba na magari ya kifahari ya washirika sita wa kibiashara wa mshukiwa mkuu katika sakata hiyo, Bi Josephine Kabura.

Hii ni kufuatia ombi lililowasilishwa na Shirika la Kutwaa Mali ya Wizi (ARA) mbele ya Jaji Mumbi Ngugi.

Miongoni mwa washukiwa hao ni; Anthony Gethi Sh3.1 milioni, mamake, Charity Gethi na dadake Jedidah Wangari Wangui.

Wengine wanaoshukiwa kufaidi kutokana na Sh791 milioni za NYS ni Sam Mwadime Sh40 milioni, John Kago (Sh273 milioni), John Ndung’u, Jame Gachoka na James Kisingo.

Shirika hilo limepatiwa idhini ya kutwaa mali hiyo. Na jana EACC ilipata idhini ya mahakama kufunga akaunti nne za benki za Mkurugenzi wa Rasilimali katika Hazina Kuu ya Kitaifa, Charles Muia Mutiso, anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Bw Mutiso anadaiwa kufuja fedha za umma kati ya Aprili 2015 na Aprili 2020.Akaunti zake za benki ya Absa, Kenya Commercial Bank (KCB) na Cooperative zina jumla ya Sh36.7 milioni.

Katika benki ya Absa, Bw Mutiso ana akaunti mbili; moja ina Sh23.4 milioni na nyingine Sh5.8 milioni.Katika benki ya Cooperative amehifadhi Sh1.9 milioni na KCB kuna Sh5.5 milioni.

“Mali aliyo nayo Bw Mutiso inaonekana kuwa nyingi kuliko mapato yake. Hata hivyo, atapewa fursa ya kujitetea huku uchunguzi ukiendelea kwa mujibu wa sheria,” ikasema taarifa ya EACC.

Tume ya kupambana na ufisadi pia inachunguza gari la Bw Mutiso na vipande vyake vitano vya ardhi vilivyoko katika Kaunti za Nairobi na Machakos.

Jaji Mumbi Ngugi aliagiza akaunti hizo zifungwe kwa kipindi cha miezi sita kuwezesha EACC kukamilisha uchunguzi wake kabla ya kuanza mchakato wa kutaifisha mali hiyo iwapo atapatikana na hatia.Hiyo inamaanisha kwamba Bw Mutiso hataweza kutoa au kuweka fedha kwenye akaunti zilizofungwa hadi Januari mwaka ujao.

Kadhalika, hataweza kuuza gari lake au vipande vyake vya ardhi vinavyochunguzwa.Kulingana na EACC, Bw Mutiso mara nyingi amekuwa akiweka fedha kwenye akaunti zake za benki kupitia ATM.

“Kwa mfano, mwezi wa Juni 2015, aliweka Sh2 milioni kwenye akaunti zake katika benki ya Absa ndani ya siku chache,” ikasema taarifa ya EACC.

Bw Mutiso alikuwa akipata mshahara wa Sh144,675.60 kila mwezi. Kati ya Aprili 1, 2015 na Aprili 30, 2020 alipokea mshahara wa jumla ya Sh7,148,991.25.

Kulingana na EACC, Mutiso alijiunga na Hazina Kuu ya Kitaifa na kuwa Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali mnamo Julai 16, 2014.

Kabla ya kujiunga na Hazina Kuu ya Kitaifa, Bw Mutiso alikuwa mwanauchumi katika Wizara ya Fedha ambapo alihudumu tangu Julai 31, 2002.