Habari

Juhudi za vijana kuokoa machifu waliotekwa Mandera zilivyotibuliwa na polisi

Na MANASE OTSIALO February 5th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

FAMILIA za machifu watano waliotekwa nyara na wapiganaji wa Al-Shabaab katika kaunti ya Mandera hazijaandikisha taarifa huku Rais William Ruto akisisitiza kuwa serikali itahakikisha maafisa hao wamepatikana wakiwa hai.

Aidha, Jumanne ilibainika kuwa baadhi ya vijana waliojitolea kuwasaka machifu hao walijeruhiwa na maafisa wa usalama.

Hali hiyo imeibua maswali kuhusu namna operesheni ya kuwaokoa machifu hao ilishirikishwa.

Rais Ruto aliahidi kuwa operesheni ya kiusalama ya kuwasaka machifu hao itaendeshwa katika maeneo yanayopakana na Somalia huku duru zikisema huenda maafisa hao wa utawala walivukishwa mpaka hadi taifa hilo jirani.

Watano hao walitekwa nyara Jumatatu asubuhi katika barabara ya Wargadud-Elwak walipokuwa safarini kuelekea makao makuu ya kaunti ndogo ya Mandera Kusini kwa shughuli za kikazi.

Akiongea mjini Mandera, Rais Ruto alisema lengo la wapiganaji hao wa Al-Shabaab lilikuwa kueneza woga katika kaunti hiyo ili asitishe ziara yake ya maendeleo.

“Al-Shabaab walitaka kuleta woga katika kaunti ya Mandera kwa kuteka nyara machifu wetu. Ninataka kuwaahidi watu wa Mandera kwamba, machifu hao sharti warejeshwe nyumbani na tutapambana na magaidi hao kwa njia zote,” akasema.

Kiongozi wa taifa alisema kuwa Naibu Inspekta Jenerali Gilbert Masengeli ataongoza operesheni ya kuwarejesha nyumbani machifu hao.

“Tuko hapa na Naibu Inspekta Jeneral Gilbert Masengeli na nimemwamuru kuhakikisha kuwa tumewakomboa machifu wetu,” akasema.

“Mashariki au Magharibi, sharti tuzime kero hili la Al-Shabaab ili watu wa kaskazini mwa Kenya waishi kwa amani,” akaongeza. Wakati wa operesheni hiyo, Rais Ruto alisema maafisa wa usalama watachambua maeneo yote kuwasaka machifu hao.

“Hatutapumzika hadi tuhakikishe kuwa kaskazini mwa Kenya ni salama kama sehemu zingine za nchi,” akaeleza.