Jumwa ashtaki wanaharakati 2 kwa kumchafulia jina
MWENYEKITI wa Bodi ya Barabara za Kenya, Bi Aisha Jumwa, amewashtaki wanaharakati wawili wa kisiasa, akidai wanamharibia sifa kwa kusambaza rekodi ya sauti yake ambapo anadaiwa kutusiana.
Kupitia kwa wakili Alfred Omwancha, Bi Jumwa anataka mahakama iagize kusitishwa kwa usambazaji wa kanda hiyo ya 2016, akiwalaumu wanaharakati Idd Salim na Matano Maingi.
Hakimu Mwandamizi wa Malindi, Bi Joy Wesonga, aliorodhesha kesi hiyo kusikizwa Septemba 10. Wakili wa washtakiwa, Bw Lucky Minyazi, aliomba mahakama impe siku tatu kujibu madai ya Bi Jumwa.