Kadi za Huduma Namba kupeanwa hivi karibuni
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA 37 milioni ambao walijisajili kwa Huduma Namba mwaka 2019 wataanza kupokea kadi hizo baada ya miezi minne.
Vilevile, serikali itaanzisha awamu ya pili ya usajili wa takriban Wakenya 10 milioni ambao hawakusajiliwa mwaka 2019.
Afisi mshirikishi wa Mfumo wa Kitaifa wa Kuhifadhi Maelezo ya Wakenya (National Integrated Identity Management System-NIIMS) Philip Lemarasia alisema serikali inasubiri bunge lipitishe sheria fulani wezeshi kabla ya kuanza kusambaza kadi hizo.
Alisema afisi yake imepata hakikisho kwamba bunge litapitisha Mswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali ya 2019 na Mswada wa Kulinda Data ya 2019 ambazo zinalenga kutoa mwongozo kuhusu matumizi ya data za kielektroniki zilizokusanya wakati wa usajili mwaka jana.
“Wakati huu tunasubiri miswada hii miwili ipitishwe na bunge na baada ya kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali tutaanza kutoa kadi za Huduma Namba kwa Wakenya. Na hii itachukua muda wa miezi minne hivi,” Bw Lemarasia alisema.
Afisa huyo alisema hayo Alhamisi katika makao makuu ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC), Nairobi wakati wa mkutano wa wadau kuhusu mpango wa usajili wa walimu kielektroniki.
Mpango wa usajili wa Huduma Namba ulisitishwa Septemba 2019 kufuatia kesi iliyowasilishwa mahakamani na ambayo uamuzi wake ulitolewa Januari 30, 2020.
Mahakama iliamua kwamba serikali haifai kuendelea na shughuli hiyo hadi pawepo na sheria mahususi ya kuongoza utekelezaji wake na kulinda data za wananchi.
“Usajili wa Huduma Namba ambao ulipaswa kuendelea ulisitishwa na mahakama kutokana na ukosefu wa sheria za kuuongoza mchakato huo. Sheria wezeshi zikipitishwa, tutaanza kusambaza kadi hizo,” Bw Lemarasia akasema.
Jumla ya Wakenya 37 milioni walisajiliwa mwaka 2019 katika shughuli iliyoendeshwa kuanzia Aprili 25 hadi Juni 14, 2019. Mpango huo uligharimu Sh8.5 bilioni.