Kagwe atishia kuagiza mahindi kutoka ng’ambo
WAZIRI wa Kilimo Mutahi Kagwe ameonya kuwa serikali itaanza kuagiza mahindi yasiyolipiwa ushuru iwapo wakulima wataendelea kuhodhi mazao yao.
Bw Kagwe alifichua kwamba serikali imetenga Sh1.7 bilioni kununua magunia milioni 1.7 ya mahindi lakini wakulima wamekataa kuwasilisha mazao haya kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).
Alitoa onyo hilo katika bohari ya NCPB Kaunti ya Kirinyaga baada ya kuzindua usambazaji wa mbolea ya bei nafuu.
Alitoa makataa ya hadi siku 30 kwa wakulima wayawasilishe mahindi yao kwa NCPB la sivyo wizara itaanza kuyaagiza bila kulipiwa ushuru nje ya nchi.
Serikali imekuwa ikinunua kila gunia kwa Sh4,000 pesa ambazo baadhi ya wakulima wanaona ni kiwango cha chini ndiposa wamehodhi mahindi wakisubiri bei ipande.