Kalombotole ashtakiwa kunyemelea wagonjwa KNH na kuwaua
MWANAMUME amefikishwa kortini kwa kuwanyemelea wagonjwa hafifu waliolazwa Hospitali Kuu ya Kenyatta na kuwaua.
Kennedy Kalombotole alifikishwa mbele ya hakimu mkazi mahakama ya Kibera Daizy Mutahi.
Alikabiliwa na shtaka la kumuua Edward Maingi Ndegwa usiku wa Julai 17, 2025 katika Orofa ya Saba –Wadi C.
Mbali na Ndegwa, mahakama ilifahamishwa Kalombotole anachunguzwa kwa mauaji ya mgonjwa mwingine mnamo Februari 6-7, 2025.
Mahakama iliombwa na afisa anayechunguza kesi hiyo Koplo Bernard Muange iamuru Kalombotole azuiliwe korokoroni kwa siku 21 kusaidia maafisa wanaochunguza visa hivyo vya mauaji.
Mahakama ilifahamishwa kwamba Kalombotole alilazwa katika hospitali ya KNH mnamo Novemba 2024.
Hakimu alifahamishwa kwamba mshukiwa huyu ni hatari kwa usalama wa wagonjwa katika KNH.
“Naomba hii mahakama iamuru Kalombotole azuiliwe kwa siku 21. Mshukiwa huyu yuko na mazoea ya kuwavamia wagonjwa waliodhoofishwa na magonjwa na kuwaua kama hakuna mmoja wao anaweza kujitetea,” kiongozi wa mashtaka alimweleza Bi Mutahi.
Mahakama iliombwa itilie maanani kwamba Kalombotole hana makazi maalum yanayojulikana kwa vile amekuwa katika KNH tangu 2024.
“Polisi wanataka kuchimba na kufahamu kiini cha Kalombotole kuwavizia wagonjwa ambao wamedhoofishwa na maradhi na kukatiza maisha yao,” Koplo Muange alidokeza.
Hakimu aliambiwa kisa hiki kililetea nchi majonzi na wasiwasi huku watu walio na changamoto za kiafya waliolazwa KNH wakihofia maisha yao.
“Naomba mahakama izingatie wasiwasi unaokumba watu walio na wagonjwa waliolazwa KNH na kuamuru Kalombotole asalie ndani ya korokoro ya polisi hadi uchunguzi dhidi yake ukamilishwe,” Koplo Muange alimsihi hakimu.
“Epusha wagonjwa na Kalombotole. Amuru azuiliwe rumande,” Koplo Muange alisihi hakimu.
Akitoa uamuzi, hakimu aliamuru Kalombotole awekwe chini ya ulinzi mkali katika kituo cha polisi cha Kilimani hadi Julai 24, 2025 atakapotoa uamuzi ikiwa atazuiliwa kwa siku 21 au la.