Habari

Kalonzo amruka Ruto Kipetero

Na ANTONY KITIMO May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amekanusha madai ya Rais William Ruto kwamba kiongozi wa nchi alimtafuta ajiunge na serikali lakini akakataa.

Bw Kalonzo alisema hajawahi kukutana na Rais Ruto kujadili suala kama hilo na badala yake alisisitiza kuwa hatawahi kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza, bali ataendelea kushinikiza ajenda ya kuhakikisha kuwa serikali ya sasa itaondoka madarakani 2027.

Katika mkutano wa faragha wa viongozi wa Ukambani uliofanyika Ikulu siku ya Jumatano, Rais Ruto alimlaumu Kalonzo Musyoka kwa kukataa kushirikiana naye huku akijitetea kwa kushirikiana na Raila. ‘Baada ya uchaguzi wa 2022, nilimwendea Bw Musyoka kabla ya Bw Odinga. Lakini alikataa na kusema alitaka kubaki katika upinzani,’ kiongozi wa nchi alisema. Hata hivyo, jana Bw Musyoka alisema hajawaji kuzungumza na Rais Ruto kuhusu suala hilo na hayuko tayari kufanya hivyo.

“Haiwezi hata kufikirika kwamba ninaweza kufanya kazi katika serikali hii. Sitaki hata kujadili jambo lolote na kiongozi wa nchi. Namheshimu lakini nitaendelea na jukumu langu kama upinzani rasmi baada ya ODM kujiunga na UDA serikalini. Nitasalia upande wa wananchi na kuokoa nafsi yangu mbele ya Wakenya na kizazi cha Gen Z,” alisema Bw Kalonzo.

Akizungumza jijini Mombasa wakati wa Mkutano Mkuu wa 42 wa Chama cha Wahasibu Kenya (ICPAK), Bw Kalonzo alisema kuwa wale walio nje ya serikali wanaandaa upinzani madhubuti kuhakikisha utawala wa Rais Ruto utafikia kikomo mwaka 2027.

“Tutafuata Katiba na tunapaswa kuchukua hatua kupambana na ufisadi na kuondoa wale walio nyuma yake. Si siri kwamba kuna uozo mkubwa nchini Kenya na kwa maoni yangu, taaluma ya uhasibu inapaswa kuhimiza uwajibikaji na uwazi katika demokrasia yenye afya,” alisema Bw Kalonzo.

Katika mkutano huo, aliwataka wahasibu wakemee serikali ya sasa kwa kunyakua mamlaka ya taasisi huru za kikatiba kama vile Ofisi ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Bajeti, pamoja na vitisho dhidi ya maafisa wanaohudumu, hasa Nancy Gathungu na Dkt Margaret Nyakang’o.

“Vitendo vya kishujaa vya Bi Gathungu na Dkt Nyakang’o katika kufichua uozo unaoendelezwa na viongozi wa sasa yanapaswa kupongezwa. Licha ya vitisho na hofu, wamesimama imara. Dhamira yao na maadili hazijatetereka. Nawaomba viongozi wa ICPAK kuunga mkono mashujaa hawa wawili wa taaluma yenu,” alisema Kalonzo.

Bw Kalonzo alisema kuna mwamko wa raia unaoenea nchini, hasa miongoni mwa vijana, na akataja matukio ya Juni 25 mwaka jana kama wakati wa mabadiliko ya kitaifa.

“Wakati vijana wa Kenya walijitokeza kwa wingi barabarani kote nchini, hawakuwa wakipinga tu Mswada wa Fedha wa 2024 wakiwa wamejihami kwa chupa ya maji, bendera ya taifa na simu zao za mkononi, walikuwa wanarejesha nafasi yao ya kushiriki katika kuunda mustakabali wa taifa letu,” alisema kiongozi huyo wa Wiper.

Aliwataka wataalamu kuwa mstari wa mbele kutoa sauti zao wakati fedha za umma zinaibwa na sera zisizotekelezeka zinapotungwa na kupitishwa.

“Ninawapa changamoto kuvuka mipaka ya kufuata sheria tu hadi kwenye kiwango cha dhamira. Sheria huuliza, Je, ni halali? Lakini dhamira huuliza, Je, ni sahihi?”

Pia aliwataka wahasibu wazungumze kuhusu mchakato wa marekebisho ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Nawasihi, kama chama wa wataalamu, msimame na kuungana na idadi inayoongezeka ya watu wanaoonyesha kutokuwa na imani na uteuzi wa Rais Ruto, na pia kuomba taarifa kamili na ya wazi kuhusu mchakato wa uteuzi kutoka kwa Kamati ya Uteuzi ya IEBC,” alisema.