Habari

Kalonzo kwa Ruto: Shauriana nasi kabla kuteua makamishna IEBC au tuwakatae

Na CHARLES WASONGA May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

UPINZANI unajiandaa kupinga majina ya Wakenya watakaoteuliwa na Rais William Ruto kushikilia nyadhifa za mwenyekiti na makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) endapo Rais William Ruto atafeli kushauriana na vinara wake kabla ya kufanya uteuzi huo.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka sasa anamtaka Dkt Ruto kushauriana — na kukubaliana — na mrengo wa upinzani kabla ya kuteua makamishna hao wa IEBC, kulingana na mapendekezo ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO).

Jumanne wiki hii, Dkt Ruto alipokea majina mawili kwa wadhifa wa mwenyekiti na mengine tisa kwa nyadhifa za makamishna wa IEBC, kutoka kwa jopo lililoendesha usaili wa kusaka watu bora kwa nyadhifa hizo.

Kwenye taarifa baada ya kupokea majina hayo, kiongozi wa taifa aliahidi kuzingatia Sheria ya IEBC ya 2024, atakapoteua mmoja kati ya wawili hao kuwa mwenyekiti na sita kati ya tisa hao kuhudumu kama makamishna wa tume hiyo.

“Kwa mujibu wa Sheria ya IEBC, nitateua na kuwasilisha majina hayo katika Bunge la Kitaifa nikizingatia misingi ya kikatiba inayoongoza mfumo wetu wa uongozi,” Dkt Ruto akasema.

Lakini saa chache baadaye, Bw Musyoka alimwandikia Rais barua akimtaka kumshauriana na kukubaliana na upinzani kabla ya kuteua watu hao, ilivyopendekezwa kwenye ripoti ya Nadco.

“Barua hii inahusu mapendekezo kwenye ripoti ya Nadco kuhusu mageuzi katika IEBC na nidhamu katika vyama vya kisiasa. Aya ya 862 inasema kuwa ili kujenga imani kwa IEBC, itakuwa muhimu kwa viongozi wa miungano hii miwili kushauriana na kukubaliana kabla ya Rais kuteua mwenyekiti na makamishna wa IEBC,” Bw Musyoka akasema katika barua hiyo.

“Ukumbuke kuwa kamati ya Nadco iliundwa kutokana maamuzi ya Bunge la Kitaifa na Seneti, Agosti 19, na Agosti 29, 2023, mtawalia. Na ripoti yake ilitokana na mazungumzo yaliyozileta pamoja mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja-One Kenya kwa nia ya kuleta uponyaji kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2022. Kamati hiyo ilipendekeza mageuzi ya kikatiba, kisheria na kisera kuhusu masuala ambayo Wakenya walilalamikia,” Bw Musyoka akaongeza.

Kwa hivyo, kulingana na kiongozi huyo wa Wiper mchakato wa uteuzi wa viongozi wa IEBC haupasi kuendeshwa na mrengo wa Kenya Kwanza pekee.

Bw Musyoka, ambaye alikuwa mwenyekiti mwenza wa kamati ya Nadco, anaonya kwamba umma utapoteza imani kwa makamishna watakaoteuliwa na Rais Ruto endapo atachelea kufanya mashauriano na upinzani.

“Aidha, hatua hiyo itaendeleza dhana kuwa wasimamizi hao wa uchaguzi wameteuliwa na mrengo wa Kenya Kwanza na hivyo hawataendesha kazi zao kwa njia huru na haki,” akaeleza.

Bw Musyoka anaongeza kuwa kwa sababu kiongozi wa ODM Raila Odinga sasa anashirikiana na serikali ya Kenya Kwanza, upinzani sasa unawakilishwa na chama chake, Wiper na Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) chake aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.

Kwa hivyo, kulingana naye, yeye na Bw Wamalwa ndio wanapasa kutambuliwa kama wawakilishi wa upinzani katika mashauriano yoyote kuhusu uteuzi wa wasimamimizi wa IEBC.

Hata hivyo, Bw Wamalwa, ambaye alikuwa mmoja wa wawakilishi wa Azimio katika kamati ya Nadco, alidinda kutia saini ripoti yake iliyotolewa rasmi Novemba 23, 2023.

Kiongozi huyo wa DAP-K alipuuzilia mbali ripoti hiyo akidai haikutoa mapendekezo kuhusu namna ya kushughulikia kero la kupanda kwa gharama ya maisha.