Kalonzo kichwa kinauma kuhusu 2027
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka anakabiliwa na maamuzi magumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, huku migawanyiko ndani ya upinzani ikitishia azma yake ya kuwania urais kwa mara ya pili.
Ingawa Bw Musyoka angependa kuidhinishwa kuwa mgombea wa urais wa upinzani, huenda akalazimika kuchagua kati ya kuendelea kusisitiza azma hiyo, kukubali kuwa mgombea mwenza wa Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna au kujiunga na Rais William Ruto.
Hata hivyo, hakuna hakikisho kwamba atapata nafasi ya mgombea mwenza iwapo atakubali wito wa kujiunga na Rais Ruto, ambaye tayari anakabiliwa na ushindani wa washirika wake, wakiwemo wanaotaka kuwania nafasi ya Naibu Rais.
Kutokuwa na makubaliano kuhusu mgombea mmoja wa upinzani wa kumenyana na Dkt Ruto kunamweka Bw Musyoka, 72, kwenye shinikizo huku baadhi ya wanasiasa wakitilia shaka uwezo wake wa kushinda urais.
Jumatatu, Dkt Ruto alitumia ziara yake Tseikuru, nyumbani kwa Bw Musyoka, kumshawishi kiongozi huyo wa Wiper ajiunge naye, akidai amekuwa akidhalilishwa na washirika wake wa kisiasa.
“Walimpitisha kwenye mahojiano 2022. Mlimwona akiulizwa kuhusu maelezo yake ya kibinafsi na mafanikio yake. Huko kulikuwa kumdhalilisha. Wale wale walioandaa mahojiano hayo mnamo 2022 wanapanga mengine hivi karibuni. Badala ya Kalonzo kuenda kwenye mahojiano mengine, anapaswa kujiunga nami,” akasema Dkt Ruto.
Wakati wa ziara hiyo, alimwelekeza mkandarasi anayejenga barabara ya Kandwia-Kyuso-Tseikuru yenye urefu wa kilomita 55 kuiongeza hadi karibu na makazi ya Bw Musyoka, kilomita tatu kutoka mji wa Tseikuru.
Bw Musyoka aliwakilisha eneobunge la Mwingi Kaskazini kuanzia 1985 hadi 2013. Aliwania urais 2007 na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Mwai Kibaki na Raila Odinga, kabla ya kumuunga mkono Raila katika chaguzi za 2013, 2017 na 2022.
Hata hivyo, baadhi ya washirika wake wanaamini bado anafaa kuwania urais, licha ya kuongezeka kwa umaarufu wa Bw Sifuna, hasa miongoni mwa vijana.
Seneta wa Kitui Enock Wambua amemshauri Bw Musyoka asikubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Sifuna, akisisitiza kuwa anatosha kuwania urais.
“Wengine watakapokubaliana kumteua, Ruto anapaswa kuanza kufunganya virago vyake kutoka Ikulu kwa sababu 2027 ndiyo nafasi yake bora zaidi,” akasema Bw Wambua katika mahojiano na Taifa Leo. Alipinga madai kuwa Bw Musyoka hakubaliki miongoni mwa vijana, akisema uzoefu wake wa muda mrefu katika siasa unamfaa kuongoza nchi.
“Wiper ina vijana, na wanaofanya kazi na Kalonzo ni vijana. Anaelewa masuala yao na anafaa kuwaongoza. Kalonzo anakidhi vigezo vyote, na tutasukuma azma yake ndani ya upinzani,” akaongeza.
Miezi mitatu iliyopita, kiongozi wa DP Justin Muturi pia alimuunga mkono Bw Musyoka kuwa mgombea wa urais wa upinzani.
“Ikiwa haitakuwa mimi, nitamuunga mkono Dkt Stephen Kalonzo Musyoka kuwa mgombea wa urais,” akasema Bw Muturi katika ibada ya kanisa Kamulu, Kaunti ya Machakos.
Wakati huo huo, uwezekano wa Bw Musyoka kuwa mgombea mwenza wa Bw Sifuna umezua mjadala ndani ya upinzani. Washirika wa kiongozi huyo wa Wiper wamepuuza madai ya aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala kwamba Bw Musyoka anapaswa kukubali nafasi hiyo katika uchaguzi wa 2027.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Bw Malala alidai kuwa kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua alikuwa amekubali kumuunga mkono Bw Sifuna katika mkutano uliofanyika nyumbani kwake Wamunyoro, Kaunti ya Nyeri.
Hata hivyo, Msemaji wa Wiper Ndegwa Njiru alipinga madai hayo, akisema Bw Malala alikuwa akijaribu kuleta mgawanyiko ndani ya upinzani.
“Matamshi yanayohusishwa na Seneta Malala yanaweza tu kuelezewa kuwa kazi ya mwandishi wa tamthilia badala ya mwanasiasa makini. Malala anaonekana kuwa na nia ya kuingiza kisu cha migawanyiko ndani ya moyo wa upinzani,” akasema.
Bw Musyoka alitoa matamshi hayo wakati wa ziara yake kwa Bw Gachagua katika makazi yake ya Wamunyoro. Katika ziara hiyo, Seneta wa Nyandarua John Methu, mshirika wa Bw Gachagua, alisema viongozi wa upinzani wanapaswa kukubaliana kuhusu mikakati ya kumshinda Dkt Ruto. “Kalonzo na Bw Gachagua wamekubaliana kwamba mtoto hatakufa mikononi mwao,” akasema Bw Methu, akimaanisha kuwa hawataruhusu juhudi zao za kumwondoa Rais mamlakani zishindwe.
Hata hivyo, si viongozi wote wanaounga mkono azma ya Bw Sifuna walio tayari kushirikiana na Bw Musyoka. Mbunge wa Bumula Wanami Wamboka, mwandani wa Bw Sifuna, hivi majuzi alisema hawako tayari kushirikiana na Bw Musyoka kwa sasa, akisisitiza kuwa wanataka kufanya kazi na eneo la Mlima Kenya na kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani.
“Hatuwezi kushirikiana na Kalonzo kwa sasa kutokana na yale aliyotufanyia kuhusu jina la Ukombozi. Kipaumbele chetu ni kufanya kazi na Mlima Kenya hadi uchaguzi, na njia pekee ya kushirikiana naye ni ikiwa upinzani utatoa mgombea mmoja wa urais, ambaye ni Sifuna,” akasema Bw Wamboka.
Kwa upande mwingine, kujiunga na Dkt Ruto kunaweza kumfungulia Bw Musyoka njia ya kuwania nafasi ya Naibu Rais. Hata hivyo, nafasi hiyo tayari inatamaniwa na ODM pamoja na washirika wa Naibu Rais Kithure Kindiki, hali inayoweza kuzidisha ushindani ndani ya kambi ya Rais.
Mhadhiri wa chuo kikuu Profesa Lumala Masibo alisema mustakabali wa Bw Musyoka utategemea uwezo wa upinzani kufikia makubaliano kuhusu mgombea na mikakati ya pamoja.
“Upinzani unahitaji kuwa na mikakati na kila kiongozi anapaswa kuwa tayari kumuunga mkono mwenzake. Ikiwa Kalonzo hatateuliwa kuwa mgombea wa urais, basi huo utakuwa mwisho wake. Akishindana na Ruto akiwa na uungwaji mkono wa upinzani au pekee yake, atashindwa vibaya. Kwa hivyo, ni bora ajiunge na Rais,” akasema Profesa Masibo.
Aliongeza kuwa Bw Musyoka anaweza kuwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto ili kuimarisha uungwaji mkono wake Ukambani na kupatanisha mirengo ya ODM na washirika wa Prof Kindiki.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo pia alisema umri, fedha na mikakati ya Bw Musyoka vinaweza kuwa changamoto, akidai kuwa hajajenga msukumo mkubwa wa kisiasa nje ya Ukambani.
“Ni rahisi zaidi kwake kujiunga na Rais, na hapaswi kumshinikiza yeyote kwa masharti magumu kwa sababu anatafuta njia ya kuendelea kuwa na nafasi katika siasa,” akasema Bw Bigambo.
Aliongeza kuwa kukubali kuwa mgombea mwenza wa Bw Sifuna kunaweza kudhoofisha hadhi ya Bw Musyoka baada ya miaka mingi katika siasa za kitaifa