Mapasta kuchangisha Sh10m kufanikisha mazishi ya waliokufa ajalini Mtito Andei
MUUNGANO wa wachungaji wa kidini Mombasa umeanzisha harambee ya kuchangisha Sh10 milioni kwa ajili ya mazishi ya wenzao watatu waliofariki katika ajali ya Mtito Andei.
Haya yanajiri huku shinikizo likiongezeka kwa serikali kujenga barabara ya Mombasa-Nairobi yenye njia mbili kila upande ili kupunguza ajali za barabarani.
Watatu hao walikuwa miongoni mwa watu 24 waliofariki Jumapili asubuhi baada ya basi lililokuwa safarini kurudi Mombasa kugongana na lori la mizigo eneo la Kanga, karibu na Mtito Andei.
“Mioyo yetu imevunjika. Kanisa liko katika majonzi, na wachungaji wanalia. Tulitumia siku mbili Mtito Andei kuwafariji waathiriwa na kutambua miili ya ndugu zetu,” Katibu Mkuu wa muungano huo, Mchungaji Elijah Waini, alisema.
Bw Waini alimshukuru Gavana wa Makueni Mutula Kilonzo Jr, ambaye utawala wake uliondoa malipo yote ya hospitali na uchunguzi wa maiti, ukahifadhi miili ya marehemu na kutoa magari ya kusafirisha miili hiyo hadi Mombasa kwa ajili ya kuhifadhiwa.
Hata hivyo, mwili mmoja wa afisa wa polisi aliyekuwa akihudumu Mikindani, ambaye pia alikuwa mhudumu wa kanisa, bado uko katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Mtito Andei.
Duru zilisema kuwa uhamisho wa mwili huo unasubiri maagizo kutoka kwa idara ya kitaifa ya huduma za polisi (NPS), ingawa Taifa Leo haingeweza kuthibitisha kutoka kwa familia ya marehemu.