Kalonzo, Matiang’i wataka serikali iwajibike ili kutuliza Gen Z
VIONGOZI wa upinzani wametaka serikali iwajibike kama njia ya pekee ya kuponya uhusiano uliovunjika kati ya utawala wa sasa na kizazi cha vijana, wakisema taifa haliwezi kuendelea mbele bila ukweli na maridhiano.
Wito wao umetolewa siku moja baada ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa maandamano ya Juni 25, 2024 ambayo imegeuka kuwa siku ya ghasia na majonzi.
Viongozi hao, akiwemo kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i, na Eugene Wamalwa, walisema kuwa matukio ya Jumatano yameonyesha wazi kuwa taifa linakumbwa na mgogoro wa uongozi ambao hauwezi kufumbiwa macho.
“Kama tunataka kusonga mbele kama taifa, hatuwezi kufanya hivyo bila kuwa wakweli. Ukweli ni lazima,” alisema Dkt Matiang’i akiwa ameandamana na viongozi wenzake.
“Hii sio Kenya tuliyoitazamia,” alisema Bw Musyoka. “Ni lazima tuendelee kulaani ukatili wa kupindukia wa polisi. Taifa limeungana kwa hasira dhidi ya serikali isiyojali.”
Katika maandamano ya Jumatano, watu zaidi ya 10 walifariki, zaidi ya 400 walijeruhiwa, na wengine 61 kukamatwa katika vituo mbalimbali vya polisi. Maandamano hayo yalifanyika katika kaunti zisizopungua 26 kote nchini.
Kulingana na ripoti ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), watu hao walifariki katika kaunti sita: wawili Machakos, wawili Makueni, na mmoja mmoja katika Kiambu, Nakuru na Nyandarua.
Viongozi hao walizungumza baada ya kuwatembelea waathiriwa waliolazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Alhamisi.
Bw Wamalwa alisema: “Tumeona kwa macho yetu wenyewe majeruhi. Wengi wao wamepigwa risasi na bado wako hospitalini.”
“Siku ya Jumatano ilipaswa kuwa siku ya kuwakumbuka waliopoteza maisha mwaka jana. Lakini badala ya maombi na heshima, tumepoteza maisha tena. Hii ni sawa na kuongeza chumvi kwenye kidonda,” aliongeza Wamalwa.
Aidha, alionya serikali dhidi ya kuruhusu siasa za makundi ya wahuni kuota mizizi nchini
Seneta wa Kisii Richard Onyonka naye alisisitiza kuwa haki lazima itendeke kwa waathiriwa wa maandamano hayo.
“Kama hakuna haki, basi kamwe hakutakuwa na amani,” alisema Bw Onyonka.