Kalonzo ni msaliti, mkabila, mwoga na adui wa handisheki – ODM
NA CECIL ODONGO
VIONGOZI wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) wamemtaja kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kama kiongozi msaliti anayeongozwa na hisia za kikabila anapomfanyia mwaniaji wa chama chake kampeni za uchaguzi mdogo wa Embakasi Kusini utakaoandaliwa Aprili 5.
Wabunge na viongozi wa ODM katika kaunti ya Nairobi walisema wako tayari kumkabili vilivyo Bw Musyoka walipowapokeza Irshad Sumra na Chris Karan vyeti vya uteuzi vya kuwania viti vya ubunge vya Embakasi Kusini na Ugenya mtawalia. Hafla hiyo iliandaliwa katika Jumba la Orange House jijini Nairobi.
Mbunge wa Makadara George Aladwa, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Bw Sumra walikemea vikali matamshi aliyoyatoa Bw Musyoka siku ya Jumanne kwamba ODM inafaa kumwachia mgombeaji wa Wiper Julius Musili Mawathe kiti hicho kwa kutowasilisha mgombeaji katika eneobunge la Embakasi Kusini.
Bw Sumra alidai Bw Musyoka anaongozwa na ukabila anapomvumisha Bw Mawathe huku akimkumbusha kwamba yeye na Bw Mawathe ni waoga waliohepa hafla ya kuapishwa kwa kinara wa NASA Raila Odinga kama rais wa wananchi mwaka uliopita.
“Kalonzo ni mkabila na tunamtaka apeleke huo ukabila wake Ukambani. Yeye na Bw Mawathe walijificha mvunguni mwa kitanda wakati Bw Odinga alipokuwa akiapishwa. Pia asifikirie kwamba tumesahau baadhi ya maamuzi yake ya kisiasa miaka ya nyuma yaliyoathiri uwezekano wa kiongozi wetu kushinda urais,” akasem Bw Sumra.
Mbunge huyo wa zamani pia alishukuru chama hicho kwa kumpa tiketi ya kupeperusha bendera yake na akaahidi kupigana kufa kupona hadi apate ushindi.
Bw Aladwa naye aliwashtumu baadhi ya wabunge wa Jubilee walioungana na Bw Musyoka kumuunga mkono Bw Mawathe akiwataja kama maadui wa salamu za maridhiano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga maarufu kama ‘handisheki’.
Mbunge huyo alimkumbusha Bw Musyoka kwamba mwaniaji wa Wiper katika eneo bunge la Lang’ata kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 ndiye alimkosesha mgombeaji wa ODM uwezo wa kutwaa kiti hicho na akamtaka kusahau uungwaji mkono kutoka kwa chama hicho siku za usoni.
“Wabunge kama Moses Kuria wanaojifanya wanatutishia kwa kuungana na Bw Musyoka ndio maadui wa Handshake. Bw Kuria aende afanye siasa zake Gatundu kwasababu hatoshi kushiriki siasa za Nairob,” akasema Bw Aladwa.
Bw Sifuna naye aliahidi kwamba chama hicho kitatumia rasilimali zake kuhakikisha kwamba Mabw Sumra na Karan wanatwaa viti vyao. Vile vile alipongeza chama cha Jubilee kwa kutowasilisha mwaniaji wa viti hivyo viwili.