Habari

Kamati yaamua kuendelea na vikao kuchambua hoja ya kumwondoa Samboja ofisini

October 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

JUHUDI za Gavana wa Taita Taveta Granton Samboja za kuzuia kamati maalum ya seneti kuchunguza sababu zilitolewa na madiwani wa kaunti hiyo kutaka afutwe kazi zimegonga mwamba Jumanne.

Kamati maalum ya seneti iliyoteuliwa kuchunguza sababu zilizotolewa na madiwani wa Taita Taveta kutaka Samboja afutwe kazi imeamua kuendelea na vikao vyake.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Njeru Ndwiga ametupilia mbali pingamizi za wakili Nelson Havi wa Gavana Samboja kuwa vikao hivyo vitishwe kwa misingi ya agizo la mahakama kuu.

Havi alitaka kamati hiyo ikome kushughulikia suala hilo hadi kesi ambayo gavana huyo aliwasilisha kortini itakaposikizwa na kuamuliwa lakini ombi likataliwa na wanachama wa kamati hiyo.

“Kwa kuzingatia majukumu ya kamati hii maalum ilivyoelezwa katika kipengele cha 33 cha Sheria ya Serikali ya Kaunti ya 2013 na sheria za seneti nambari 75, nakuzingatia maagizo ya naibu spika, kamati hii inatupilia mbali pingamizi hizo na inaamua kuendelea na vikao vyake namna ilivyopangwa,” Seneta Ndwiga akasema Jumanne.

Awali, wakili Havi alikuwa ameiambia kamati hiyo kwamba sheria za bunge la seneti hazikupaswa kushughulikiwa kwa sababu ya agizo la mahakama lililotolewa na Jaji Weldon Korir Oktoba 17 kukomesha vikao vya kusikizwa kwa madai dhidi ya Bw Samboja.

“Tuliwasilisha agizo hilo la mahakama katika ofisi ya Karani wa Seneti Jeremiah Nyengenye na katika bunge la Kaunti ya Taita Taveta kwamba mchakato wa kumwondoa mteja wangu ofisini usitishwe. Hili linakubalika kwa mujibu wa sheria za seneti nambari 95 (1) na (2),” akasema Bw Havi.

Wakili huyo alisema bunge la Kaunti ya Taita Taveta lilipitisha hoja ya kumwondoa Samboja mamlakani bila kumpatia nafasi ya kujitetea wala kumfahamisha kuhusu mashtaka dhidi yake.

“Hii ni kinyume cha hitaji la sheria kwamba mshtakiwa apaswa kupewa nafasi ya kujitetea dhidi ya mashtaka dhidi yake kabla ya uamuzi kutolewa,” akasema Bw Havi.

Uhuru

Lakini Bw Ndwiga alisema sheria za seneti nambari 95 (5) zinampa Spika uhuru wa kuamua ikiwa bunge hilo linaweza kushughulikia suala liliwasilishwa mahakamani au la.

“Kwa hivyo, tumepata idhini kutoka kwa ofisi ya Spika kwamba tuendelee na vikao vya kusikiza na kuchambua suala hili hadi mwisho,” akasema huku akiungwa mkono na wakili wa bunge la kaunti ya Taita Taveta Charles Njenga.

Kamati hiyo ya wanachama 11 sasa imesalia na siku tisa kushughulikia suala hilo kabla ya kuandaa ripoti yake yenye mapendekezo ya kuunga mkono au kupinga madai yaliyomo katika hoja iliyopitishwa na madiwani wa Taita Taveta wiki jana.

Miongoni mwa sababu za kumwondoa gavana Samboja ofisini kulingana na hoja hiyo ni kwamba Bw Samboja alikiuka Katiba kwa kudinda kuidhinisha bajeti ya kaunti hiyo.

Vilevile, madiwani hao wanadai kuwa serikali ya Gavana Samboja imefeli kuwasilisha michango ya wafanyakazi wa kaunti hiyo katika hazina za kulinda masilahi yao.

“Licha ya serikali ya Kaunti ya Taita Taveta kukata michango ya wafanyakazi za Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF) na Hazina ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) pesa hizo hazijakuwa zikiwasilishwa katika taasisi hizo. Hii ni kinyume cha sheria na inaiweka masilahi ya wafanyakazi hatarini,” akasema diwani Hariss Keke aliyedhamini hoja hiyo.

Madiwani hao pia walimsuta Bw Samboja kwa kile walidai ni kuwahadaa wakazi wa Kaunti ya Taita Taveta alipokusanya sahihi zao 52,000 kwa kwa ajili ya kuanzisha mchakato wa kuvunja kaunti hiyo.