Kamati ya Bajeti yakausha wizara, yasema hazitaongezewa fedha
WIZARA za serikali zitaendelea kupungukiwa na fedha baada ya Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti kusema hazitaongezewa fedha zingine ikizingatiwa kuwa kuna pengo la Sh876.1 bilioni katika bajeti ijayo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Samuel Atandi, Alhamisi (Mei 22, 2025) alisema upungufu wa mgao wa fedha ndilo suala kuu linaloikabili kamati hiyo inapopokea mapendekezo kutoka kwa kamati za bunge zinazochunguza matumizi ya fedha katika wizara mbali mbali za serikali
Mbunge huyo wa Alego Usonga alisema japo pengo la Sh876.1 bilioni kwenye bajeti ni la chini zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma makisio ya kiwango cha ukusanyaji mapato yaliyotolewa na Wizara ya Fedha sio sahihi.
“Sisi kama wanachama wa kamati hii tutaendesha shughuli zetu katika mazingira magumu zaidi kwa misingi ya upungufu uliopo kwenye bajeti,” Bw Atandi akasema.
“Hatuna nafasi ya kufanya lolote. Maombi ya fedha zaidi yaliyowasilishwa na Wizara, Idara na Mashirika ya Sekali hayatakubaliwa,” akasisitiza.
Bw Atandi alisema hayo wakati wa kikao cha kwanza cha kamati hiyo cha kupokea ripoti kuhusu changanuzi za makadirio ya bajeti kutoka Wizara, Idara na Mashirika (MDAs) ya serikali katika mwaka ujao wa kifedha wa 2025/2026.
Karibu kamati zote za bunge zimepokea maombo kutoka MDAs zikitaka ziongezewe mgao wa fedha, zikidai kuwa mgao wa umepunguzwa ikilinganishwa na mgao wa bajeti ya 2025/2026.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Leba Ken Chonga alilalamikia mgao finyu wa fedha kwa Idara ya Leba na Upanuzi wa Ujuzi ambayo bajeti yake imepunguzwa kwa kima cha Sh1.1 bilioni, akipendekeza kuwa pesa hizo zirejeshwe.
Afisa ya Bunge kuhusu Bajeti (PBO) inayowashauri wabunge kuhusu masuala ya bajeti iliambia kamati ya bajeti kwamba Wizara ya Fedha imeahidi kukopa Sh592.1 bilioni kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini na Sh284 bilioni kutoka nje kuziba pengo kwenye bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/2026.
Wizara ya Fedha imesema kuwa bajeti ya mwaka huo wa kifedha ni ya kima cha Sh3.36 trilioni ambapo Sh1.7 trilioni ni za matumizi ya kawaida na Sh707 bilioni zitatumika katika miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti wa zamani wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Ndindi Nyoro alilalamikia kile alichodai ni mjama ya Wizara ya Fedha kuvuruga makadirio ya upungufu katika bajeri kwa lengo la kuchukua mikopo kutoka nje.