Habari

Kamera za CCTV zahusisha maafisa wa benki na kuporwa, kuuawa kwa mteja Mumias

Na SHABAN MAKOKHA April 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAAFISA kutoka Idara ya Uchunguzi kuhusu Uhalifu (DCI) wamezidisha uchunguzi kuhusu kisa ambapo mwalimu wa kike aliporwa na kuuawa baada ya kutoa pesa kutoka benki moja mjini Mumias.

Makachero wanawalenga washukiwa wanne wakiwemo maafisa wawili wa benki. Bi Akinyi, kutoka kijiji cha Budonga, Navakholo, alishambuliwa na kunyang’anywa Sh285,000 kabla ya kuuawa.

Kumeibuka mtindo wa kuhofisha mjini Mumias ambapo wateja wanaotoa chochote zaidi ya Sh100, 000 wanalengwa ghafla na majambazi wanaowaandama kwa gari au pikipiki na kuwaibia katika kinachoonekana sasa kuwa genge la wahalifu lililojipanga vyema linalohusisha hata waajiriwa wa benki.

Bw Nthiga alisema wafanyakazi wawili wa benki waliomhudumia mwalimu ni washukiwa kufuatia picha za CCTV zilizonaswa na kamera za usalama katika benki hiyo.

“Hatulegezi Kamba kuwaandama waliomwibia na kumuua mwalimu. Tuna vidokezo muhimu kutokana na rekodi za CCTV kutoka benki hiyo zinazotusaidia kuwatambulisha washukiwa zaidi,” alisema Bw Nthiga.

Wapelelezi wanawaandama wanaume wengine wawili walioonyeshwa na kamera za CCTV wakiwasiliana na wahudumu na mlinzi wa benki kwa njia ya kutiliwa shaka.